Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro (wa pili kushoto) akimkabidhi tuzo ya shukrani Mkuu wa Kitengo cha Bima wa Benki ya NMB, Bw. Martin Massawe (wa pili kulia) kwenye hafla ya Uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Soko la Bima kwa Mwaka 2022 iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Balozi wa Bima, Bi. Zena Saidi na Mwenyekiti wa Bodi ya Bima, CPA. Moremi Marwa wakifuatilia tukio hilo.
SERIKALI imeagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) kwa kushirikiana na wadau wengine wa bima kuhakikisha vifurushi vya bima ya afya kwa wote vinakuwa rahisi na rafiki kwa watanzania wote kumudu.
Aidha, imewataka waendelee kuimarisha mikakati ya kuendeleza sekta ya bima sambamba na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kidigitali.
Aidha, watoa huduma wa bima wametakiwa kuimarisha matumizi ya teknolojia ili kusimamia na kukuza bidhaa zao kwa urahisi zaidi.
Akitoa maelekezo hayo leo Dar es Salaam, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro amesema elimu kuhusu bima bado changamoto hivyo, wadau wote wachukue changamoto hiyo na kueleza umuhimu wa bima kwa wakati huu ambao serikali imepitisha sheria ya bima ya afya kwa wote.
Amesema watanzania wanahitaji elimu zaidi ili waweze kunufaika na bima hiyo.
"Bima ya afya kwa wote ni safari ya miaka 21 hivyo tuhakikishe tunatumia ipasavyo haki hii sawa kwa watu wote, hivyo mnadi na kutoa elimu package zenu na ziwe rahisi kwa watanzania wote kumudu," amesisitiza Dkt. Ndumbaro
Ameongeza kuwa mamlaka hiyo inapaswa kuhakikishe wananchi wanapata huduma zinazokusudiwa kwa haki sawa na haraka.
Pamoja na hayo, amesema wadau wa sekta ndogo wanapaswa wajiepushe na ubadhilifu ikiwemo matumizi ya bima feki ambayo hurudisha nyuma maendeleo ya nchi na kwamba vitendo hivyo ni jinai na ichukue hatua kwa wanaoshiriki vitendo hivyo.
Amesisitiza kuwa wanahitaji kubuni bidhaa mpya za bima zitakazokidhi mahitaji ya soko kwani kazi yake ni kulinda mali na maisha.
"Ni muhimu kubuni bidhaa mpya na kuanzisha mifumo ya malalamiko ili kutoa matokeo ndani ya muda mfupi na kuondoa makosa ya kiufundi," amesema.
Ameongeza kuwa "Takwimu za miaka mitano 2018/22 zinaonesha kuwa sekta hii inakuwa hivyo muhakikishe mnakuwa zaidi na kuongeza pato la taifa ili watanzania wawe salama zaidi."
TIRA katika kutekeleza majukumu yake huongozwa na mpango Mkuu wa maendeleo wa sekta ya fedha kwa mwaka 2019/20 hadi 2028/29, Mpango wa maendeleo wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 na Ilani na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa upande wake, Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware amesema soko la bima limekuwa na kufikia trilioni 1.158 kwa mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asimilia 26.7 huku mwaka 2021 mapato yote yalikuwa shilingi bilioni 911 ambapo yameongezeka na kufikia kiwango hicho cha juu yaani trilioni 1.158.
“Niyashukuru sana makampuni ya bima kwa kazi nzuri mlioifanya kwa kipindi hicho, bima za kawaida zimeongezeka kutoka bilioni 746 mwaka 2021 mpaka bilioni 895 mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.9.
Amesema katika nchi zilizowekeza kwenye soko la bima nchini, Tanzania inaongoza sokoni kwa asilimia 69.9, ikifuatia na Kenya 20.9, Afrika Kusini 3.5, Botswana 1.8, Zambia 1.8, Uswisi 1.8, Uingereza 0.5, Ujerumani 0.4, Canada 0.3 na Mauritania 0.2.
Ameongeza kuwa, wameanzisha bima ya mpango wa kilimo ili kuwahusisha wakulima ambao ni asilimia 65 ya nguvu kazi ya taifa.
Pamoja na mambo mengin, Tira pia wamezindua muongozo wa usimamizi wa ubakizaji wa bima Mtawanyo sambamba na kuzitunuku baadhi ya kampuni zilizofanya vizuri kwa kuwafikia watu wengi zaidi.
No comments:
Post a Comment