HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 1, 2023

Mshauri wa Kodi Kizimbani kwa Tuhuma za Kuisababishia TRA Hasara

 Na Karama Kenyunko Michuzi tv

MSHAURI wa Kodi, Denis Tililo (29) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es salaam akikabiliwa na mashtaka nane likiwemo la utakatishaji na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh milioni 118.9.

Tililo ambaye ni mshauri wa kodi wa kujitegemea, anayeishi eneo la Msingwa Dar es Salaam, amesomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Rehema Lyana leo Novemba Mosi 2023 jijini Dar es Salaam.

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa serikali Theresia Mtao akisadiana na Auni Chilamula na Emmanuel Medalakini kutoka TRA amedai katika kesi hiyo mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka sita ya kutoa risiti za uongo kutoka kwenye mashine ya Kielektroniki (EFD), kuisababishia Mamlaka ya mapato Tanzania TRA hasara na utakatishaji fedha zaidi ya sh. Milioni 100.

Mbele Hakimu lyana inadaiwa Agosti 28, mwaka huu maeneo ya Buguruni wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, mshtakiwa Tililo alitoa risiti ya uongo kutoka kwenye mashine ya EFD iliyosajiliwa kwa jina la Yasini Revelian kwa nia ya kumdanganya Kamishna Mkuu wa TRA kwa ajili ya kumlipa mfanyabiashara hewa aitwae Janeth Kitego mwenye Namba ya Mlipakodi (TIN) namba 143-472-604 Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Sh milioni 7.6.

Pia mshtakiwa huyo anadaiwa kutoa risiti ya uongo yenye namba 342 kutoka kwenye mashine ya EFD iliyosajiliwa kwa jina la Revelian kwa lengo la kumdanganya Kamishina Mkuu kumlipa Kitego VAT ya Sh milioni 30.5.

Mshauri huyo wa kodi anadaiwa kutoa risiti ya uongo namba 343 kutoka kwenye mashine hiyo iliyosajiliwa kwa jina la Revelian na kumdanganya Kamishna Mkuu kumlipa Kitego VAT ya Sh 27,457,627.12.

Wakili Mtao alidai Tililo alitoa risiti ya uongo ya namba 343 kupitia mashine hiyo ya EFD ya Revelian kwa lengo la kumdanganya Kamishna Mkuu kuwa anamlipa mfanyabiashara hewa ambaye ni Kitego mwenye TIN namba 143-472-604 VAT ya Sh milioni 27.4/-

Katika mashtaka mengine inadaiwa mshtakiwa alitoa risiti ya uongo namba 344 kwa kutumia mashine hiyo yenye kiasi cha Sh. milioni 780 na kupotosha mfumo wa kodi wa TRA kwa lengo la kumdanganya Kamishna ili kumlipa Kitego VAT ya Sh 118,983,050.85.

Imeendelea kudaiwa kuwa ni kinyume na sheria na kwa makusudi aliisababishia TRA hasara ya Sh. milioni 118.9 kwa kutoa risiti za uongo ambazo zilikuwa zinalenga kutoa taarifa za uongo kwa Kamishina pamoja na mfumo wa mamlaka hiyo.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, Tililo anadaiwa kufanya miamala ya fedha ya Sh. 118,983,050.85 wakati akijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa la uhalifu la kutumia risiti zisizo halali.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kikodi katika kesi hiyo bado haujakamilika hivyo, wameiomba mahakama kuipangia kesi hiyo tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Lyana ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 14, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kumtaka mshitakiwa kurudi rumande kwa kuwa mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kwamba moja ya shtaka linalomkabili la utakatishaji halina dhamana.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad