HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 9, 2023

BASHUNGWA AAGIZA TBA KUONGEZA KASI UKUSANYAJI MADENI

 WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amewataka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuongeza bidii ya ukusanyaji wa madeni kwa wapangaji wao na kuweka mikakati itakayowawezesha kukusanya madeni hayo ili kupata fedha za kujenga nyumba nyingine za kisasa na kuwezesha watumishi wengi wa umma kupata huduma ya nyumba na makazi bora.


Hatua hiyo inafuatia kutoridhishwa na kasi ya ukusanyaji madeni iliyopo sasa katika majengo yake nchini kote.

Akizungumza katika kikao kazi na Menejimenti ya TBA, Waziri huyo ameutaka Wakala huo kuandaa kanzi data ya majengo yote inayoyamiliki na viwanja nchini kote ili kuisimamia kikamilifu na hivyo kuwawezesha kuja thamani ya mali iliyopo.

“Mtendaji Mkuu nataka kuona jitihada yenu katika ukusanyaji wa madeni yote mnayodai, hakikisheni madeni yanalipwa kwa wakati bila kujali nani anayedaiwa, amesema Bashungwa.

Waziri Bashungwa ameagiza Wakala huo kuhakikisha kuwa mtazamo uliopo makao makuu ya TBA katika kukusanya madeni, kubuni miradi mipya ya kisasa na kuwaelimisha watumishi uwepo katika mikoa yote ili miradi ya ujenzi wa kisasa ifanyike na kodi zikusanywe kikamilifu na kuipa TBA hadhi inayostahili.

Waziri huyo amezungumzia TBA kusimamia kikamilifu mali za Serikali na kuzikagua kila wakati ili ziwe kwenye ubora wakati wote na kukidhi malengo na matarajio ya Serikali kwa Wakala huo.

Ameitaka TBA kutoa huduma bila upendeleo ili kuwawezesha viongozi na watumishi wa kawaida kunufaika na nyumba hizo.

“Ongezeni ubunifu na kushirikiana na Taasisi nyingine katika kujenga miradi mikubwa kwenye maeneo ya kimakakati na yenye mahitaji makubwa ya makazi na biashara ili kupata tija kwa wakala huo na Serikali kwa ujumla”, amesema Bashungwa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, amemueleza Waziri Bashungwa kuwa TBA itaendelea kutekeleza maelekezo yake na kuyatolea taarifa katika kila kipindi cha robo mwaka ili kufikia matarajio ya Wizara na Serikali.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akizungumza na Wakurugenzi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), katika kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma, Novemba 09,2023.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad