HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 18, 2023

WANNE KIZIMBANI WAKIDAIWA KUIHUJUMU TRA ZAIDI YA MILIONI 590

  

Wafanyabiashara wanne wanaoishi jijini Dar Es Salaam, wakiingia katika  Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam leo Oktoba 18, 2023 wakikabiliwa na mashitaka sita likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh. Milioni 592.3


WAFANYABIASHARA wanne wanaoishi jijini Dar Es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakikabiliwa na mashitaka sita likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh. Milioni 592.3

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na jopo la wakili wa serikali wanne wakiongozwa na wakili wa serikali Mwandamizi Grolia Mwenda imewataja washitakiwa hao kuwa ni Salum Mbegu (38) Mkazi Wa Majohe Mji Mpya, Peter Ntikula (27) Mkazi Wa Buguruni, Baraka Ntikula (37) Mkazi Wa Mkuranga Na Hamad Hamad.

Wakili Mwenda alisaidiana kusoma mashtaka dhidi ya washtakiwa na wakili wa serikali, Upendo Mono, Medalakini Emmanuel Na Hauni Chilamula Mbele Ya Hakimu Mfawidhi, Susan Kihawa.

Mashtaka mengine wanayowakabiliwa nayo washtakiwa ni Kuongoza genge la uhalifu, kutumia mashine za Kielektroniki za EFD kwa lengo la kuharibu mfumo na kumdanganya Kamishna, kutoa risiti zisizo halali za EFD na kukutwa na mali ya wizi au iliyopatikana kinyume cha sheria.

Inadaiwa, kati ya mwaka 2018 na Oktoba 3 mwaka huu, huko Buguruni Kisiwani, ndani ya Wilaya ya Ilala, jijini Dar Es Salaam, washtakiwa kwa lengo la kujipatia faida, waliongoza genge la uhalifu kwa kutumia mashine ya EFD kuharibu mfumo, kumdanganya Kamishna na kutoa risiti zisizo halali.

Pia inadaiwa katika tarehe hizo, washitakiwa hao walitumia mashine za EFD kwa lengo la kupotosha mfumo kwa kutoa risiti zisizo halali na kuziingiza kwenye mfumo wa TRA na kusababisha Mamlaka hiyo kudaiwa kodi ya ongezeko La Thamani (VAT) ya Sh 592,336,714.

Washitakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutoa risiti bandia za EFD kwa nia ya kumdanganya kamishna na walipa kodi kudai kodi ya ongezeko La thamani (VAT) kinyume cha Sheria.

Katika shtaka la nne inadaiwa, Oktoba 3, mwaka huu washitakiwa Mbegu, Ntiluka Na Baraka, Walikutwa na mashine tano Za EFD ambazo walizipata kinyume cha Sheria.

Aidha, kati ya mwaka 2018 na Oktoba 3 mwaka huu, washitakiwa kwa pamoja waliisababishia TRA hasara ya Sh. Milioni 592.3 kwa kutoa risiti zisizo halali.

Mwenda ameendelea kudai kuwa, katika shtaka la Utakatishaji fedha washitakiwa wote wanadaiwa kuhusika kutoa muamala wa Sh Milioni 592.3 Wakati wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu.

Hata hivyo washtakiwa wamekana kutenda kosa hilo na wamerudishwa rumande kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida husikilizwa mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 30, 2023 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad