HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 26, 2023

TCD WAZINDUA JUKWAA LA WANAWAKE WA VYAMA VYA SIASA

 

 Mwenyekiti wa TCD, Profesa Ibrahim Lipumba na viongozi wengine wakipiga makofi baada ya kuzindua jukwaa la Majadiliano la Wanawake wa Vyama vya Siasa taifa kwaajili ya kukuza nafasi ya ushiriki wa Wanawake katika Siasa na michakato ya Uchaguzi. Jukwaa hilo limezinduliwa jijini Dar es Salaam leo Oktoba 26, 2023
Mwenyekiti wa TCD, Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza wakati wa kuzindua jukwaa la Majadiliano la Wanawake wa Vyama vya Siasa taifa kwaajili ya kukuza nafasi ya ushiriki wa Wanawake katika Siasa na michakato ya Uchaguzi. Jukwaa hilo limezinduliwa jijini Dar es Salaam leo Oktoba 26, 2023
Picha za pamoja.


Matukio mbalimbali.

Na Avila Kakingo, Michuzi TV
KITUO Cha Demokrasia Tanzania (TCD) leo Oktoba 26, 2023 kimezindua jukwaa la Majadiliano la Wanawake wa Vyama vya Siasa taifa kwaajili ya kukuza nafasi ya ushiriki wa Wanawake katika Siasa na michakato ya Uchaguzi.

Jukwaa hilo limezinduliwa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa TCD, Profesa Ibrahim Lipumba kwa kushirikiana na viongozi wa Vyama vya siasa pamoja na Mabalozi wa Uswis na Marekani Nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Lipumba amesema jukwaa hilo litaimarisha usalama wa wanawake pale wanapowania nafasi mbalimbali za uongozi katika vyama, uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

Pia litasaidia kufanyia kazi mapendekezo ya wanawake kuhusiana na masuala ya maendeleo endelevu yanayowahusu katika vyama pamoja na serikali kwa ujumla na kuongeza nafasi ya ushiriki na ushirikishwaji wa mambo ya siasa pale zinapotokea nafasi za kugombea katika chaguzi mbalimbali na zile za vyama vyao.

"Jukwaa hili litaongeza ufahamu wamasuala ya kisiasa kwa wanawake kwani wanatakiwa kujiamini ili waweze kufikia hatua ya kushika Nyadhifa mbalimbali za kisiasa katika vyama kisiasa na Serikali". Amesema Prof. Lipumba

Prof. Lipumba amesema katika mwelekeo wa serikali kufanya mchakato wa kutoa dira mpya ya maendeleo endelevu ya taifa wanawake wanahitajika zaidi kutoa maoni yao yatakayochangia kupatikana kwa dira yenye mahitaji muhimu kwaajili ya kumsaidia mwanamke kimaendeleo.

Amesema, Jukwaa hilo litakuwa na kazi ya kuwaunganisha wanawake wa vyama vya siasa na kushirikiana kwa kuhamasishana kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika vyama na serikali na kufanya maamuzi ya msingi na kuweza kuchagua watu wanaofaa na kuhakikisha kwamba mambo yanayowavusha wanawake yanakuwa mbele katika sera za Sheria.

Pia Prof. Lipumba amesema kuwa jambo la muhimu ni kuweza kujenga msingi wa demokrasia utakaowajengea uwezo Wanawake kushiriki katika shughuli za kidemokrasia chaguzi za kisiasa, kupiga kura lakini pia kama wagombea wa nafasi mbalimbali.

Akizungumzia kuhusiana hali ya demokrasia nchini kama inatoa uwanja kwa Wanawake kushiriki katika siasa, Prof. Lipumba amesema kuwa kwa sasa usawa wa jinsia unazingatiwa kwani Wanawake wanamfano wa kuiga kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa kama chaguzi kuwa za huru na haki ushiriki wa Wanawake utakuwa Mkubwa.

Kwa Upande wa Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Didier Chassot, amesema uwakilishi wa wanawake katika Bunge la Uswisi bado uko mbali na kuakisi uhalisia wa idadi ya watu, ambapo wanawake huhesabiwa kulingana na idadi ya watu.

Amesema Wanawake bado wanakabiliwa na changamoto linapokuja suala la malipo sawa na uwakilishi sawa katika nafasi za uwajibikaji, katika sekta ya umma na ya kibinafsi.

Usawa wa kijinsia ni muhimu kwa maendeleo kama ilivyoelezwa na lengo la tano la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, "Usawa wa kijinsia sio tu haki ya msingi ya binadamu, lakini msingi wa lazima kwa ulimwengu wa amani, ustawi na endelevu".

Pia ameipongeza Tanzania kwa hatua iliyofikiwa katika kupunguza pengo la kijinsia, kama inavyoonyeshwa lakini ripoti ya Pengo la Jinsia Duniani, ripoti inayotolewa kila mwaka na Jukwaa la Uchumi la Dunia ambalo hupima usawa wa kijinsia duniani kote.

Amesema Tanzania imeboresha nafasi yake katika Pengo la Jinsia Duniani, ikitoka nafasi ya 60 kati ya nchi 146 zilizofanyiwa tathmini mwaka jana hadi nafasi ya 45. maendeleo chanya yamesajiliwa katika ngazi ya uwezeshaji wa kisiasa, huku wanawake wengi zaidi wakiteuliwa kushika nyadhifa za uwaziri kutoka 18% mwaka 2022 hadi 30% mwaka 2023.

Kwa upande wake katibu wa Jumuiya ya Wanawake kutoka CUF na Mwakilishi wa Jukwaa la Wanawake, Anna Riaba amesema wanawake wa vyama vya siasa wanakabiliwa na changamoto zinazofana.

Wanawake wa Vyama vya siasa walioshiriki katika uzinduzi huo ni kutoka CCM, CHADEMA, ACT-WAZALENDO, NCCR - Mageuzi, Chama cha Ukombozi wa Umma na CUF.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad