HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, October 22, 2023

SERIKALI YAFURAHIA MWENENDO WA PUMA ENERGY TANZANIA KATIKA BIASHARA YA MAFUTA NCHINI

 

 

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati imesema imekuwa ikifurahishwa na mwenendo mzuri wa Kampuni ya Mafuta Puma Tanzania ambayo inajihusisha na biashara ya mafuta, gesi na vilainishi na kubwa zaidi imekuwa na bunifu zenye kuleta tija katika biashara ya sekta ya mafuta nchini.

Miongoni mwa ubunifu huo ni pamoja na kuwatambua na kutoa zawadi kwa waendeshaji bora wa vituo vya mafuta vilivyo chini ya kampuni hiyo nchi nzima ambao wanafanya vizuri zaidi katika kuwahudumia watanzania katika  maeneo mbalimbali 

Hayo yamesemwa  Oktoba 20, 2023 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa NIshati Judith Kapinga wakati wa hafla ya kuwatambua, kuwatangaza na kuwapa zawadi waendeshaji  bora wa vituo vya mafuta vya Puma Energy nchini kwa mwaka 2023.

Naibu Waziri Kapinga amesema huduma bora ndizo zinazoifanya 
kampuni hiyo iendelee kuwa namba moja kwa utoaji wa huduma za mafuta nchini, hivyo Serikali itaendelea kuiunga mkono kuhakikisha inaendelea kuwa katika ubora unaotakiwa na kuiletea nchi mapato zaidi.

"Kwa mujibu wa taarifa za Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Puma Energy Tanzani ni kiongozi wa soko katika usambazaji na uuzaji wa bidhaa za mafuta ya petrol nchini.

"Kutokana na ubora wake Puma Energy Tanzania imeendelea kuaminiwa kutoa huduma za mafuta katika miradi mingi ya kimkakati ya Serikali ukiwamo ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere na mradi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR).

"Hivyo nakupeni hamasa ya kuendelea kuchangamkia fursa hizo ambazo kipekee zinachagizwa na utayari wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo imeendelea kuboresha mazingira mazuri ya uwekezaji."

 Pamoja na hayo Naibu Waziri Kapinga ameitaika Puma Energy Tanzania kuendelea kupanua wigo wa ujenzi wa vituo vya mafuta hususan katika maeneo ya pembezoni miji

"Licha ya kuwa na jumla ya vituo 74 kwa nchi nzima lakini ukiangalia ukubwa wa kampuni hii vituo hivyo ni idadi ndogo sana, ongezeni juhudi na kujenga vituo katika sehemu mbalimbali za nchi hususan vijijini.

"Mnafahamu mafuta ni changamoto katika baadhi ya maeneo watu wanabeba madumu, hivyo tunawapa shime kuendelea kuongeza vituo. Najua mmesema mmeongeza vituo viwili lakini ningependa mwende mbele zaidi hususan kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa."

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania Fatma Abdalla amesema mafanikio ya kampuni hiyo yanatokana na kazi nzuri inayofanywa na watoa huduma wao waliopo katika vituo mbalimbali nchini.

Amesema wamekuwa wakiwapatia wateja wao huduma iliyobora kila wanapotembela vituoni huku akifafanua kwamba watoa huduma hao ndilo jicho la kampuni hiyo.

Amesema lengo la kampuni hiyo ni kuwapa huduma bora Watanzania kufikia malengo yao katika maisha hivyo wataendelea kuboresha huduma kulingana na wakati na mahitaji huku akieleza mkakati wao ni kuwa na vituo vya mafuta 120 katika muda mfupi ujao.

Katika tuzo hizo Kituo cha Mafuta Cha Puma Arusha kiliibuka mshindi wa kwanza huku kituo cha mafuta cha Puma Upanga  jijini Dar es Salaam ikitwaa nafasi pili kwa kutoa  huduma bora kwa wateja.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Puma Energy Tanzania Dk. Seleman Majige ambaye katika salamu zake aliahidi kampuni hiyo kufanyia kazi maelekezo ya Serikali yaliyotolewa na Naibu Waziri Judith kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo.

Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga( wa tatu kushoto) akimkabidhi tuzo Mkurugenzi wa Kituo cha Mafuta cha Puma  Arusha,Husin Sjat baada ya kuibuka mshindi wa kwanza wa tuzo za  Puma Energy Tanzania mwaka 2023.Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Puma Dk.Seleman Majige na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Puma nchini Tanzania Fatma Abdallah. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad