HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 18, 2023

Sekta ya usafirishaji Nchini Inahitaji Wataalamu wa Kutosha - Prof Mbarawa

 WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema sekta ya usafirishaji nchini bado inahitaji, wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kufanya kazi katika miradi ya kimkakati inayoendelea ili kuendana na kasi ya ukuaji katika sekta hiyo.


Pia amewataka wadau wa sekta hiyo kuendelea kufanya tafiti zitakazoboresha usafirishaji kwani uendeshaji wake unategemea kupata takwimu sahihi zitokanazo na tafiti.

Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo Oktoba 18, 2023 jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mkutano wa kwanza wa Kimataifa wa usafirishaji na usambazaji ulioandaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Amesema, ili kufanikisha malengo hayo, wanahitajika wataalamu ambao wametayarishwa vizuri na sio waliopikwa nusunusu.

Amesema ili kuendeleza miradi hiyo wanahitajika wafanyakazi na wataalam na hivyo amewataka NIT kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi, kutayarisha wataalam wazuri ambao wataitoa nchi kutoka mahali ilipo na kukuza uchumi kwa wananchi wetu ambao kwa kiasi kikubwa wanategemea sekta ya usafirisha

"Serikali imewekeza kwenye miradi mbalimbali, uwekezaji ambao unaendana na tafiti kutoka kwa wataalamu sambamba na kuwajengea uwezo watanzania kufanya kazi katika miradi hiyo" amesema Mbarawa.

Aidha Waziri Mbarawa ameipongeza NIT kwa kuandaa mkutano huo na kuongeza kuwa, hakuna nchi duniani inayoweza kuendelea kama haina sekta mahiri ya usafirishaji kwa mfano, mizigo itakuja hapa Dar es Salaam lazima iwafikie watanzania mbalimbali,’’ alisema Profesa Mbarawa.

Ameeleza kuwa mkutano huo umekutanisha wadau kutoka nchi za Marekani, Uingereza na Australia hivyo, wanaamini watapata mapendekezo mazuri na kama serikali watayafanyia kazi.

"Tumesaini mkataba wa Sh bilioni 630 kwa ajili ya kujenga karakara ya meli katika bandari ya Kigoma, kwa kujenga meli mbili kwa ajili ya kusafirisha mizigo na meli moja itakuwa na uwezo wa kubeba tani 3,500 ambayo itasafiri kupitia Ziwa Tanganyika na meli ya pili itasafiri Ziwa Victoria ikiwa na uwezo wa kubeba tani 3,000,’’ amesema.

Waziri huyo alisema ni mara ya kwanza katika historia kuwahi kujenga kiwanda kamili chenye vifaa vyote vya kisasa vinavyohusika na ujenzi wa meli na alitoa mfano wa kiwanda cha Afrika Marine cha Mombasa na Kampuni ya Secco kwamba wana viwanda hivyo lakini havina vifaa vya kisasa kwa sababu ni vya zamani.

''Tunaenda kuanzisha utaratibu wa door to door transport mfanyabiashara wa Congo akichukua biashara yake hapa anaingiza kwenye gari kutoka hapa hadi kigoma akifika kigoma anaingiza hiyo gari kwenye meli hadi Congo,'' alifafanua.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema, taasisi za elimu ya juu zina majukumu matatu ikiwemo kufundisha, kufanya utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu hivyo kupitia mkutano huo, watafiti watatoa matokeo ya tafiti walizozifanya kwa kushirikiana na nchi zilizoendelea.

Amesema, mkutano huo unakwenda kutoa majibu au takwimu zitakazowafanya wanaoendesha mashirika mbalimbali ya uchukuzi hapa nchini kama vile Shirika la Reli Tanzania (TRC), Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), kuifanya sekta ya uchukuzi na usafirishaji iweze kufanya utendaji wenye tija na kuleta matumaini makubwa ya serikali yetu liyowekeza katika sekta hii ni kuona huduma nzuri katika sekta ya usafirishaji inazidi kuimarika huduma nzuri katika usafirishaji,''amesema.

Profesa Mganilwa amesema utafiti ndiyo uliowasaidia kuanzisha programu mpya ikiwemo mitaala ya wataalamu wa reli kuanzia wahandisi hadi menejimenti ya mashirika ya reli.
WAZIRI wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akizungumza leo Oktoba 18, 2023 jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mkutano wa kwanza wa Kimataifa wa usafirishaji na usambazaji ulioandaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Mkuu wa Chuo chaNIT, Profesa Zacharia Mganilwa akizungumza leo Oktoba 18, 2023 jijini Dar es Salaam, wakati wa kufungua mkutano wa kwanza wa Kimataifa wa usafirishaji na usambazaji ulioandaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Baadhi ya wadau wa Usafirishaji wakiwa katika  wakati Ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Kimataifa wa usafirishaji na usambazaji ulioandaliwa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).


Picha za Pamoja.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad