HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 13, 2023

RC KUNENGE AAGIZA KUKAMATWA VIONGOZI 24 WALIOHUSIKA KUUZWA ENEO LA HEKA 4000 MALI YA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI KIBAHA

 Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge akizungumza kwenye mkutano na wananchi wa eneo la Mitamba Kata ya Pangani Wilayani Kibaha leo Oktoba 13,2023.





Baadhi  ya wananchi wanaodaiwa kuvamia katika eneo hilo la Mitamba.

Na Khadija Kalili, Michuzi Tv 
MKUU wa Mkoa wa Pwani Alhaj Abubakari Kunenge ametoa muda wa siku 14 kukamatwa viongozi 24 wakiwemo Mabalozi, Wenyeviti wa Mitaa, Watendaji walioshirikiana na madalali waliohusika kuwauzia wananchi viwanja katika eneo la shamba namba 34 la Mitamba lilopo Kata ya Pangani ambalo ni mali ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

RC Kunenge amesema kuwa anayo orodha ya majina ya viongozi na madalali waliohusika kuwauzia kinyemela wananchi viwanja katika eneo hilo ambalo linamilikiwa na Serikali na kwamba anayakabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), pamoja na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani (RPC), kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Mkuu wa Mkoa huyo, ametoa maagizo hayo leo Oktoba 13, 2023 wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo hilo la Mitamba lililopo Kata ya Pangani uliowahusisha watalaam kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha na Mkoa kwa ajili ya kutoa msimamo wa serikali kuhusu maamuzi ya eneo hilo ambalo limevamiwa na wananchi kwa ajili ya makazi.

Aidha Kunenge ametoa muda wa siku 60 tu kwa Halmashauri ya Mji Kibaha, kupima eneo la shamba 34 la Mitamba lenye ukubwa wa hekta 4,000 na kubainisha mipaka yote na matumizi yake ili ijulikane kama vile eneo la ujenzi wa ofisi za umma na huduma za kijamii, makazi na viwanda kabla ya kuanza oparesheni ya kuwaondoa wananchi walio ndani ya shamba hilo.

“ Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani pamoja na Kamanda wa TAKUKURU Pwani ninayo majina 24 ya viongozi na madalali waliohusika kuwauzia wananchi eneo hilo la shamba namba 34 kinyemela, wahojiwe na sheria ichukue mkondo wake,” amesema RC Kunenge.

Aidha amewataka wananchi wote waliouziwa viwanja katika eneo hilo kufungua kesi dhidi ya waliowauzia na kwamba serikali itatoa ushirikiano ikiwemo kuwatafutia mawakili wa kuwatetea.

Aidha RC huyo amefafanua kuwa majina ya waliyolipwa fidia kwa wananchi ili kupisha eneo hilo yapo ambapo walilipwa fidia na kuainishwa kuwa eneo la Hekta 2963 zimerejeshwa kwa Halmashauri kwa ajili ya kutumika kwenye shughuli za maendeleo na kubakiwa na eneo la Hekta 1037 ambazo hadi sasa zimebaki kwa ajili ya kutolewa maamuzi.

“Wananchi mjiandae tunasubiri maamuzi ya kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha kuridhia kuhusu matumizi ya eneo hili na baada ya watalaam kumega na kuyaainisha maeneo kwa ajili ya shughuli za umma, taasisi na viwanda mtapaswa kuondoka lakini eneo litakalotengwa kwa ajili ya makazi basi mtauziwa, nawaomba kwa hiyari yenu muanze kuvunja nyumba zenu wenyewe ili kunusuru vifaa mbavyo mtaona vitawafaa katika maeneo yenu mapya kuliko kusubiri kuvunjiwa.

Akizungumzia historia ya eneo hilo, Mpimaji Ardhi Halmashauri ya Mji Kibaha, Aron Shushu, amesema kuwa kiwanja hicho kimepimwa upya kwa kuzingatia sheria namba 8 ya mipango miji na kwamba mwaka 2021 kilifanyika kikao na wananchi hao kwa ajili ya kutoa katazo la kutovamia shamba hilo.

Aidha Shushu amesema kuwa jitihada za kuwakataza wanchi hao ziliendelea huku baadhi wakionekana kuendelea na shughuli za ujenzi ila wamekaidi.

Amesema kuwa wamepokea mapendekezo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu upimaji wa eneo hilo ambapo Hekta 150 zimetolewa kwa ajili ya matumizi ya Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania (TVLA), Hekta 188 kwa ajili ya matumizi ya Taasisi za Umma, 486 uwekezaji wa viwanda na 200 makazi.

Akizungumzia kuhusu uamuzi huo, Mwenyekiti Mtaa wa Lumumba mahali lilipo shamba hilo, Gideon Tairo, amewaomba wananchi kutoa ushirikiano pindi wataalam watakapofika kupima eneo hilo wasiwafanyie vurugu za aina yoyote.

Tairo amemshukuru Mkuu wa Mkoa, Kunenge kwa busara aliyoitumia kuwaelewesha wananchi kuhusu eneo hilo na kwamba wapo tayari kufuata utaratibu utakowekwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad