HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, October 1, 2023

MAWAKALA WA MASHINE ZA EFD WAFURAHISHWA NA MABORESHO

 Mwakilishi wa kampuni ya Radix inayosambaza mashine za EFD, Dorah Lusingu, akizungumza na waandishi wa habari Septemba 30, 2023 Jijini Dar es Salaam


MAWAKALA wanaosambaza mashine za kutoa risiti za kielektroniki (EFD), wamesema mashine hizio zimeboreshwa na sasa zinaweza kutoa risiti zaidi ya moja kwa mahitaji ya mteja hata pale mteja anapopoteza risiti yake.

Mabadiriko hayo ambayo yaliwavuta watu wengi kujifunza yamekuwa ya mafanikio katika wiki ya EFD iliyokuwa inaendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kwa lengo la kutoa elimu ya kodi kwa wananchi.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Jakaya Kikwete, jijini Dar es Salaam Septemba 30, 2023 wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya EFD, mawakala hao wamesema toleo la sasa la EFD linampa nafasi mfanyabiashara kutoa risiti laini kwa njia ya mtandao na ngumu, ulingana na urahisi wa mteja.

Mwakilishi wa kampuni ya Radix, Dorah Lusingu amesema TRA imerahisisha upatikanaji wa mashine hizo na kwamba zinatolewa bure kwa wafanyabiashara ambao wanarudishiwa fedha ya manunuzi kupitia ritani zao za mwaka.

Amesema, mashine hizo zinarahisisha utunzaji wa kumbukumbu za mauzo na kuepusha mtu kuwekewa makadirio makubwa ya kodi kwa kuwezesha afisa wa TRA kukadiria kilicho sahihi.

"Mashine za Radix zinaweka rekodi kuanzia mzigo unapoingia stoo hadi mauzo yake, ikiwa mfanyabiashara atatumia mashine yake ya EFD kwa uaminifu" amesema Dorah.

Naye, Mkurugenzi na mwanzishi wa aplikesheni ya EFD mtandao ya Mojatax, Timothy Maeda, amesema TRA imeidhinisha matumizi ya risiti laini ili kutoa uwanja mpana kwa wafanyabiashara kuchagua njia ya kutoa risiti ili kutimiza malengo ya nchi kupata mapato.

“Mojatax inawawezesha wafanyabishara wakubwa kwa wadogo kutoa risiti, huduma hii inarahisisha utoaji wa risiti na uvumbuzi huu unalenga kuwawezesha kufuatilia mauzo popote walipo,” amesema.

Amesema kwa wafanyabiashara wanaohitaji risiti ngumu wanaweza kutoa nakala kwa mteja japokuwa Mojatax inatoa zaidi risiti laini.

Maeda amesema EFD hiyo inapatikana kwenye simu janja na kwamba imeondoa malalamiko ya baadhi ya wafanyabishara waliokuwa wanashindwa kumudu bei ya mashine nyingine za kutolea risiti.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa kampuni ya Advatech inayosambaza mashine za EFD, Josephine Mwandambo, amesema mabadiliko ya kiteknolojia yamerahisisha utoaji wa risiti kwa njia mbalimbali ikiwamo laini na ngumu.

Meneja wa EFD wa kampuni ya Softnet, Salum Kambangwa, amesema kampuni hiyo inatoa usaidizi wa kimtandao kwa wafanyabiashara wanaonunua mashine kwenye kampuni hiyo.

Amesema mashine za kampuni hiyo zinatoa ripoti ya mauzo kwa njia ya ujumbe mfupi kwenye simu ya mmiliki wa biashara kila siku na hivyo kurahisisha kutunza kumbukumbu ya mauzo.

Anasema ripoti hiyo inamwezesha mfanyabiashara kushughulikia tatizo pale inapotokea amekosea kutoa risiti ya mauzo kwa mteja bila kujua.

“Unakuta bahati mbaya badala ya kutoa risiti ya Sh. 100,000 unatoa ya Sh. 10,000,000…unapopata ripoti ya mauzo yako ya kila siku utabaini kwamba jana hukuuza mzigo wa zaidi ya Sh. milioni 10, utaitatua shida yako haraka na utaondoa mgogoro baina yako na TRA,” amesema.

Mwakilishi wa kampuni ya Zalongwa, Rehema Chingwele, amesema wanatengeneza mifumo ya kidigitali ya EFD inayomwezesha mfanyabiashara kutoa risiti popote alipo na kufuatilia mauzo akiwa nje ya biashara yake.

“Mfanyabiashara akiwa na mfumo huu hawezi kusema mtandao wa TRA unasumbua au mashine kuharibika kwa kuwa kila kitu kinakuwa dijitali, mteja wetu akiwa na mtandao anaweza kutoa risiti bila shida yoyote,” amesema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad