HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 25, 2023

FILAMU ZA TANZANIA ZAENDELEA KUNG'ARA KIMATAIFA

Na Shamimu Nyaki
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imepokea na kujadili majukumu ya Bodi ya Filamu Tanzania na kuipongeza Bodi hiyo kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji kazi za filamu hapa nchini ambayo yamesaidia kuongeza ajira kwa Watanzania.

Akiwasilisha taarifa kuhusu Bodi hiyo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema Tasnia hiyo imeitangaza nchi Kimataifa akizitaja filamu za Tanzania zilizofanya vizuri kuwa ni Vuta Nkuvute ya Amil Shivaji ambayo imeshinda Tuzo 14 zikiwemo za nchini Marekani na Ujerumani.

Amezitaja filamu nyingine zilizofanya vizuri Kimataifa kuwa ni Jua Kali iliyofanya vizuri nchini Zambia, Binti Jasiri nchini Nigeria na Nyara nchini Nigeria.
"Bodi imeendelea kulea wasanii na kusimamia haki zao ambapo katika malalamiko 83 yaliyopokelewa na Bodi 81 yamefanyiwa kazi, ambapo wale wanaofanya vizuri tumekua tukiwatuza kupitia Tuzo za filamu za kila mwaka ambazo tayari zimefanyika kwa mara mbili na mwaka huu zitafayika mwezi Novemba" amesema Mhe. Mwinjuma

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Husna Sekiboko ameitaka Wizara iendelee kusimamia vyema utengenezaji wa Filamu Bora, zinazoitangaza Tanzania na mandhari yake pamoja na kulinda maadili ya nchi.
Kwa upande wao Wajumbe wa Kamati hiyo wakichangia taarifa hiyo  kwa nyakati tofauti wameshauri Serikali iendelee kuwatambua na kuwapa nafasi wasanii chipukizi katika majukwaa ya Kimataifa pamoja na kuongeza upatikanaji wa mafunzo kwa Wadau wao ili wafanye vizuri na kuhimili ushindani katika soko la Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad