HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 31, 2023

SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UBUNIFU NI NGUZO MUHIMU YA KILIMO

 

 

31/10/2023 Nairobi Sayansi

Imeelezwa kuwa changamoto zote zinazoikabili Sekta ya Kilimo na
Wakulima Duniani katika kuongeza uzalishaji zinahitaji matumizi ya
Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ili kuongeza tija.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof.
Adolf Mkenda wakati akitoa salamu za Tanzania kwenye Mkutano wa
Teknolojia za Kilimo Afrika Unaoendelea Jijini Nairobi nchini Kenya na
kuwakutanisha wadau zaidi 300 kutoka pande zote za Dunia.

“Changamoto kubwa ya kilimo chetu ni uzalishaji mdogo unaotokana na
sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi,Magonjwa na
Wadudu zinaweza kupata ufumbuzi kwa kutumia Sayansi Teknolojia na
Ubunifu” Alifafanua Prof. Mkenda.

Aidha amesema kuwa baada ya teknolojia hizo kupatikana ni muhimu
kuwahimiza wakulima kuzitumia kwa usahihi ili ziweze kuwasaidia
kuzalisha kwa tija na kuinua uchumi wa mkulima mmoja mmoja na Taifa
kwa ujumla.

Kwa upande wake Rais wa Zamani wa Nigeria Mhe. Dkt. Goodluck
Jonathan amesema swala la matumizi ya Sayansi katika kutafuta ufumbuzi
wa changamoto za wakulima lilianza miaka mingi na tangu miaka hiyo
Wanasayansi wanabuni na kuvumbua mpya lakini matumizi yake kwa
wakulima yamekuwa madogo.

“Ni muhimu sasa kuhimiza ubunifu wa teknolojia bora na za kisasa lakini
tusisahau kuwahimiza wakulima kuzitumia katika mnyororo mzima wa
thamani wa kilimo ili afrika iondokane na changamoto za uhaba wa chakula
kwa watu wake” alifafanua Mhe. Dkt. Jonathan.

Katika hatua nyingine ameshauri swala la uhimizaji wa vijana kushiriki
katika kilimo na kuwa ugumu wa vijana kushiriki ni kutokana na mazingira
kutokuwa rafiki kwao na kuonekana kama sio biashara bali ni cha kujikimu
pekee.

Awali akifungua mkutano huo Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Ufugaji
Mhe. Mithika Linturi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya watu wa Kenya
Mhe. Dkt. William Ruto amesema matumizi ya STI yatasaidia kilimo
kuwavutia vijana na hivyo kutoa ajira kwa watu wengi Afrika.

“Kama mnavyofahamu, kilimo ni sekta kubwa barani humo kwa mchango
wake katika maendeleo ya kiuchumi, utoaji wa ajira na malighafi kwa
viwanda vinavyotegemea kilimo. Sekta hii inachangia 23% ya mapato
katika bara huku bidhaa za msingi za kilimo zikiwakilisha sehemu kubwa
ya biashara ya Afrika, kikanda na kimataifa” alieleza Mhe. Linturi.

Aliongeza “Bidhaa za kilimo, kwa mfano, zinajumuisha takriban 65% ya
kiasi cha biashara ya ndani ya kikanda katika ukanda wa Afrika Mashariki
na kutoa ajira kwa mamilioni ya watu, kutengeneza ajira, kusaidia maisha,
na kuendesha ukuaji wa viwanda na uchumi”.

Amesema Serikali ya Rais Ruto inatambua kuwa kilimo kinalipa kwa
haraka uwekezaji unaowekwa kwani kina uwezo mkubwa wa kuzalisha
mapato ya juu kwa watu na kutengeneza fursa za ajira, Lakini ili kufungua
uwezo huu, lazima wakubali Teknolojia mpya na Ubunifu.

Amesema mkutano huo wa ACAT unafanyika wakati nchi nyingi barani
Afrika zinakabiliwa na changamoto ya kulisha idadi ya watu inayoongezeka,
inayokadiriwa kufikia zaidi ya bilioni 1.4 ifikapo 2030.

Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Kenya
kupitia Wizara yake ya Kilimo na maendeleo ya Ufugaji na Taasisi ya
Teknolojia za Kilimo Afrika AATF na unawakutanisha wadau wa kilimo
kutoka afrika na pande zote za Dunia.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda
wakati akitoa salamu za Tanzania kwenye Mkutano huo wa ACAT.
Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Dkt. Goodluck Jonathan ambaye pia ni
Balozi wa AATF akitoa neno kwenye mkutano huo.
Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Ufugaji wa Kenya Mhe. Mithika Linturi akitoa hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Rais wa Kenya Mhe. Dkt.William Ruto.








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad