WAKULIMA WA MBAAZI WA KIJIJI CHA ANGALIA WAUZA KILO MILIONI 1.9 ZILIZOWAINGIZIA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 3.7 KATIKA MNADA WA TATU WILAYANI TUNDURU - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 1, 2023

WAKULIMA WA MBAAZI WA KIJIJI CHA ANGALIA WAUZA KILO MILIONI 1.9 ZILIZOWAINGIZIA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 3.7 KATIKA MNADA WA TATU WILAYANI TUNDURU

 Na Muhidin Amri, Tunduru

WAKULIMA wa zao la mbaazi kijiji cha Angalia wilayani Tunduru,wamepata jumla ya Sh.bilioni 3,758,933,562.00 baada ya kuuza kilo milioni 1,928,872 katika mnada wa tatu uliofanyika katika Chama cha msingi(Amcos) cha Mshikamano wilayani Tunduru.

Katika mnada huo jumla ya makapuni 20 yalijitokeza kununua mbaazi,hata hivyo makampuni 6 ndiyo yaliyopata ridhaa ya wakulima ambapo bei kwa kilo moja ilikuwa Sh.1,948.

Akizungumza na wakulima wa zao hilo Mrajisi msaidizi wa ushirika mkoa wa Ruvuma Peja Mhoja alisema,kwa kuwa zao mbaazi linafanya vizuri kwa kupata soko la uhakika, ni vyema wakulima kuongeza ukubwa wa mashamba yao ili kujihakikishia mavuno mengi katika msimu ujao.

Amewataka kuacha kushikilia mbaazi majumbani,badala yake wazipeleke kwenye maghala ya vyama vya msingi kwa ajili ya kuuza kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umeonesha mafanikio makubwa tangu ulipoanzishwa.

Alisema,hatua hiyo itasaidia kuwahi soko kwa sababu baadhi ya mikoa mingine hapa nchini ambayo ni maarufu katika uzalishaji wa zao hilo itaanza kufungua masoko,hivyo itakuwa vigumu kwao kuendelea kuuza mbaazi kwa bei nzuri.

Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu Ltd)Mussa Manjaule,amewahimiza wakulima wa zao la mbaazi na mazao mengine ya kimkakati kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani na kuepuka kupeleka mazao kwa matapeli wanaonunua kwa bei isiyolingana na gharama za uzalishaji.

“tangu mfumo wa stakabadhi ghalani ulipoanza umeonyesha mafanikio makubwa kwa wakulima tofauti na soko hulia ambalo sehemu kubwa walionufaika ni wafanyabiashara wa kati,nawaombeni sana endeleeni kuuza mazao yenu kupitia mfumo huu”alisema Manjaule.

Kwa upande wake Afisa mazao wa wilaya ya Tunduru Gallus Makwisha,amevipongeza vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)na chama kikuu cha Ushirika(Tamcu Ltd) kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika uendeshaji wake.

Makwisa,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kuwathamini wakulima kwa kuendelea kutoa pembejeo za ruzuku ambazo zimesaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara katika wilaya hiyo.

Hata hivyo,amewaonya wananchi wa kijiji cha Angalia na wilaya ya Tunduru kwa ujumla,kuhakikisha wanatunza chakula walichovuna katika msimu wa kilimo 2022/2023 ili kiwasaidie kwa matumizi ya familia zao na kuepuka kuuza kutokana na tamaa ya kupata fedha.

Alisema kuwa,serikali haitakuwa tayari kutoa chakula cha msaada kwa wananchi walio bahatika kuvuna chakula cha kutosha,lakini kwa uzembe wao wameuza chakula hata kile ambacho kingewasaidia kuwafikisha hadi msimu mwingine.

Naye Afisa ushirika wa wilaya hiyo George Bisan,amewashauri wakulima kutumia fedha wanazopata kupitia shughuli za kilimo kubadili maisha yao ikiwemo kujenga nyumba za kisasa na kupeleka watoto wao shule badala ya kuishi katika nyumba za nyasi na kutumia fedha hizo kwenye mambo ya anasa.

Bisan amewataka vijana kubadilika kifikra kwa kuona kilimo kama adhabu,badala yake wachangamkie fursa zilizopo kwenye kilimo ili waweze kujikomboa na umaskini.

Mwakilishi wa wakulima wa kijiji hicho Mohamed Jana alisema,zao la mbaazi kwa sasa limekuwa tumaini jipya kwa wakulima kutokana na kuwa na soko la uhakika na bei nzuri ambayo imehamasisha wananchi wengi hasa vijana kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
Wawakilishi wa wakulima wa mbaazi wa kijiji cha Angalia wilayani Tunduru,wakisoma bei zilizotolewa na makampuni yaliyoomba kununua mbaazi katika mnada wa tatu wa zao hilo.
Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Angalia wilayani Tunduru wakifuatilia uendeshaji wa mnada wa zao la mbaazi uliofanyika katika ghala la chama cha msingi cha Ushirika Mshikamano.
Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Mussa Manjaule akifungua mnada wa tatu wa zao mbaazi katika kijiji cha Angalia wilayani humo jana,katikati Afisa Ushirika wa wilaya George Bisan.

Mrajisi msaidizi wa Ushirika mkoa wa Ruvuma Peja Mhoja akizungumza na wakulima wa kijiji cha Angalia wilayani Tunduru baada ya kukamilika kwa mnada wa tatu wa zao la mbaazi ambapo jumla ya kilo milioni 1,928,872 zenye thamani ya Sh.bilioni 3,758,933,562.00 ziliuzwa,katikati mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu Ltd)Mussa Manjaule.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad