HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 29, 2023

KLINIKI YA KWANZA YA BINAFSI YA KUTOA HUDUMA ZA MAGONJWA YA DAMU NA VIPIMO VYA MAABARA, YAZINDULIWA NCHINI

 

Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Profesa Paschal Lugajo na Balozi wa Ubalozi wa Marekani hapa nchini, David Concer wakikata utepe kuashiria Uzinduzi wa kliniki maalumu ya magonjwa ya damu (haematolojia). Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 29, 2023.

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV 
KAMPUNI ya Serenox Afrika imezindua kliniki maalumu ya magonjwa ya damu (haematolojia) ikiwemo saratani na vipimo vya maabara itayoenda kufanya utambuzi sahihi na kwa wakati kwa wagonjwa wenye matatizo hayo.

Kliniki hiyo nchini Tanzania iliyoanzishwa 2023 na Profesa Anna Schuh kutoka Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza na Dkt. William Mawalla, Mtaalamu wa haematolojia kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Shirikishi Muhimbili - (MUHAS) imezinduliwa leo Septemba 29,2023 Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Mawalla amesema, kliniki hiyo imebobea na kujikita kwenye kuhudumia wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa ya damu ambayo ni Saratani na yale yasiyo saratani ikiwemo upungufu wa damu kama vile selimundu, kuvuja kwa damu, damu kuganda kwenye mishipa, magonjwa yanayoshambulia uloto na saratani ya damu kwa watoto na watu wazima.

"Kliniki hii inafanya kazi kwa msingi kwamba utambuzi sahihi na wa wakati ni muhimu katika kutoa matibabu sahihi kwa mgonjwa sahihi na wakati sahihi." Amesema Dkt. Mawala.

"Tuna furaha kuizindua Serenox Africa na kutoa huduma zetu kwa watu wa Tanzania," "Tunaahidi kutoa huduma za utambuzi wa haematolojia zenye ubora wa hali ya juu na nafuu kwa wagonjwa wote, bila kujali asili yao au uwezo wao wa kulipia. 

Pia tunaamini kuwa kazi yetu itasaidia kuboresha uelewa wa magonjwa ya damu katika Afrika Kusini mwa Sahara na kusababisha maendeleo ya mikakati bora ya kuzuia na kutibu."

Ameongeza kuwa mpaka sasa kuna mahitaji makubwa kwa huduma kama hizo ambapo 47% ya idadi ya watu duniani hawana au wana upatikanaji mdogo wa uchunguzi wa magonjwa ya damu. 

Dkt. Mawala amesema kuwa garama za matibabu katika kliniki hiyo ni rahisi kuliko hospitali zingine zozote binafsi na wagonjwa wanaweza kufika bila kuwa na miadi yoyote na daktari.

Naye, Profesa Schuh amesema, utambuzi sahihi ni muhimu katika kutoa matibabu sahihi kwa mgonjwa sahihi na wakati sahihi... hata hivyo, 47% ya idadi ya watu duniani hawana au wana upatikanaji mdogo wa uchunguzi wa magonjwa". Amesema.

Amesema, katika Afrika, kusini mwa Sahara, magonjwa mengi ambayo yanaweza kutibiwa au kudhibitiwa vizuri kwa matibabu nafuu huchelewa kutambuliwa na hivyo kupelekea vifo hasa kwa watoto. 

Amesema asilimia 95 ya watoto wenye ugonjwa wa seli mundu hufariki  kabla ya miaka mitano ya kwanza ya maisha kutokana na kuchelewa kutambuliwa kwa ugonjwa na kwamba iwapo wagonjwa watatambuliwa mapem basi zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wanaweza kupona.

"Serenox Africa imeanzisha kituo hiki cha upimaji kwa makundi ya wagonjwa wanaosahaulika nchini Tanzania ili kutoa utambuzi mapema wa saratani kwa wagonjwa walio katika hatari kubwa na hatimaye itapanua huduma zake kwa sehemu nyingine za Afrika". Amesema Profesa Schuch

Kwa Upande wa Dkt. Lulu Chirande mhadhiri na Mtaalamu wa Haematolojia na Saratani kwa Watoto (MUHAS) amesema umuhimu wa utambuzi sahihi na wa wakati ni muhimu  katika matibabu ya watoto wenye saratani na magonjwa ya damu. Wagonjwa wengi wanafika Hospitali ugonjwa ukiwa katika hatua mbaya.  

Amesema iwapo ugonjwa utatambuliwa mapema unaweza kuepusha vifo na madhara kwani huwezi kuanza matibabu mpaka pale unapokuwa na uhakika na kile unachotibu.

Aidha Serenox katikati kuhakikisha inatimiza lengo lake la kutoa utambuzi na matibabu ya kawaida na maalum yaliyo na upatikanaji, haki na endelevu kwa watu wenye magonjwa ya damu na utambuzi wa mapema wa kansa watatoa huduma kwa bei nafuu kwa wagonjwa wanaojilipia wenyewe.

Pia watatoa huduma kwa wagonjwa wa sekta ya umma na vituo vya afya kwa gharama za maabara na huduma za kliniki na kushiriki kikamilifu katika ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi na Mashirika ya Afya ya Serikali ya Tanzania.
Mtaalamu wa haematolojia kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Shirikishi Muhimbili - (MUHAS), Dkt. William Mawalla akizungumza wakati wa Uzinduzi wa kliniki maalumu ya magonjwa ya damu (haematolojia). Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 29, 2023.
Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Shirikishi Muhimbili - (MUHAS), Profesa Bruno Sunguya akizungumza wakati wa Uzinduzi wa kliniki maalumu ya magonjwa ya damu (haematolojia). Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 29, 2023.




Matukio Mbalimbali wakati wa Uzinduzi wa kliniki maalumu ya magonjwa ya damu (haematolojia). Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 29, 2023.
Picha ya pamoja wakazi wa Uzinduzi wa kliniki maalumu ya magonjwa ya damu (haematolojia). Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo Septemba 29, 2023.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad