TAASISI ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imezindua Dawati la Jinsia kwa lengo la kuzuia vitendo vya ukatili na kushughulikia matukio yote yanayoripotiwa na wanafunzi, watumishi na wafanyakazi wengine.
Dawati hilo limezinduliwa leo na Mratibu wa Madawati ya Jinsia kwenye taasisi za elimu ya juu na Vyuo vya kati wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Gift Msowoya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Msowoya alisema matukio ya ukatili wa jinsia yalikuwa yakiendelea vyuoni lakini hakukuwa na sehemu za kutolewa taarifa.
Amesema kuwa kuanzishwa kwa dawati hilo lengo ni kuwa na mfumo rafiki wa kutoa taarifa za ukatili.
"Mnapaswa kuwa na ofisi yenye usiri itakayomfanya mtu yoyote kutoa taarifa za ukatili bila woga, muwe pia na namba ya simu ili kupokea taarifa za ukatili wakati wowote," amesema Msowoya.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo inapaswa kuunda klabu za ukatili wa jinsia za wanafunzi ili kusaidia upatikanaji wa taarifa na kutolifabya dawati hilo la watu binafsi.
"Dawati lisiwe kwa ajili ya kuangamiza watumishi, wanafunzi na wafanyakazi wengine bali mfuate sheria na taratibu zilizowekwa lakini pia kila mtumishi afanye kazi yake au masomo kwa kufuata taratibu," amesema.
Ameongeza kuwa : "Utandawazi umekuwa changamoto kubwa kwa wanafunzi wengi wao wanaingiwa tamaa na kujikuta wakifanyiwa vitendo vya ukatili hivyo muwasaidie kubadili mitazamo yao wasione maisha rahisi kwani mwisho wake ni mbaya."
Amesisitiza kuwa dawati hilo linapaswa kusaidia kunyanyua kizazi cha kujitambua na kuiokoa nchi katika kufikia dira ya dunia ya maendeleo ya kutokuendelea kwa vitendo vya ukatili.
Aidha, ameeleza taasisi kutenga bajeti kwa ajili ya madawati hayo na kutoa ripoti kila robo tatu ya mwaka.
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Taasisi Taaaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Profesa Ezekiel Amri amesema uzinduzi wa dawati hilo sambamba na uwepo wa sera utaongeza chachu katika kutekeleza kwa ufanisi sera ya taifa ya kukabiliana na ukatili.
Amesema kupitia dawati hilo wanalenga kutoa elimu ya ukatili wa jinsia kwa wafanyakazi, wanafunzi na watoa huduma wote wa taasisi, kuendesha semina za ukatili wa jinsia kwa wanafunzi na kushirikiana na madawati na taasisi za kuzuia ukatili wa jinsia.
Pia amesema watakuwa na utaratibu kuelimisha masuala ya ukatili, kutoa takwimu kuanisha matatizo hayo na kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha usawa wa jinsia kwa wanafunzi na wafanyakazi wote.
Mary Kidima alisema ukatili wa kijinsia una tabia ya kujirudia, hivyo haipaswi kuvumiliwa badala yake wahusika watoe taarifa ili iweze kushughulikiwa kwa wakati.
Alisema kuwa changamoto zinazohafifisha juhudi za taasisi kufikia malengo ya utendaji katika eneo hili ni pamoja na uelewa mdogo wa baadhi ya wanajamii kuhusu dawati la jinsia ambapo wengi wanaamini kuwa linalenga kuwatetea watu wa jinsia ya kike peke yao na limekaa kiuanaharakati.
" Ukatili wa kijinsia unaweza kufanywa na yeyote mwanaume dhidi ya mwanamke au mwanamke dhidi ya mwanaume, ndio maana dawati linashughulika na jinsia zote. Wahanga wengi wa ukatili wa kijinsia ni waoga wa kutoa taarifa na hata ushahidi pale inapohitajika hivyo tatizo linaendelea kukua bila wahusika kuchukuliwa hatua yoyote," amesisitiza Kidima.
Kauli mbiu ya uzinduzi huo ni Vunja Ukimya, Fichua Ukatili wa Kijinsia' ikitoa wito kwa wanajamii wote kutofumbia macho vitendo hivyo..
Friday, September 15, 2023
Home
Unlabelled
DIT YAZINDUA DAWATI LA JINSIA KWA LENGO LA KUZUIA VITENDO VYA UKATILI
DIT YAZINDUA DAWATI LA JINSIA KWA LENGO LA KUZUIA VITENDO VYA UKATILI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment