CMSA YAZINDUA MAUZO YA HATIFUNGANI YA BENKI YA CRDB,YASEMA ITAWEZESHA UTEKELEZAJI MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO SEKTA YA FEDHA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 31, 2023

CMSA YAZINDUA MAUZO YA HATIFUNGANI YA BENKI YA CRDB,YASEMA ITAWEZESHA UTEKELEZAJI MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO SEKTA YA FEDHA

 
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV.


MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imezindua mauzo ya Hatifungani ya Benki ya CRDB yenye mguso wa matokeo chanya kwa mazingira na jamii.

Akizungumza leo Agosti 31, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mauzo ya hatifungani ya CRDB , Mkurugenzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CPA.Nicodemus Mkama amesema uzinduzi wa mauzo ya hatifungani hiyo una thamani ya Sh.bilioni 780 sawa na dola za Marekani milioni 300.

Akielezea zaidi amesema hatifungani ya CRDB ilipata idhini ya CMSA Agosti 18, 2023, na 28 Agosti 28, 2023, CMSA ilitoa taarifa rasmi kwa umma Benki ya CRDB imepata idhini ya CMSA kutoa hatifungani yenye thamani ya Sh.bilioni 780 itakayowezesha kupata fedha za kutekeleza miradi ya kuhifadhi mazingira na yenye matokeo chanya kwa jamii.

Amefafanua hatifungani hiyo inakuwa ya kwanza kwa ukubwa ikiwa imetolewa katika fedha za aina mbalimbali na yenye mguso kwenye mazingira, na matokeo chanya kwa jamii Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Amesisitiza idhini imetolewa na CMSA baada ya Benki ya CRDB kukidhi matakwa ya Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania, Miongozo ya Masoko ya Mitaji na Dhamana ya Utoaji wa Hatifungani.

Pia uwepo wa Muundo wa Hatifungani ulioandaliwa na CRDB kwa kushirikiana na Taasisi ya Uendelezaji wa Sekta za Fedha Barani Afrika (FSD Africa) na kukidhi matakwa ya Kanuni za Jumuiya ya Kimataifa ya Masoko ya Mitaji(ICMA) na kupata ithibati kutoka kwa kampuni ya Sustainalytics ya nchini Uingereza, yenye utaalam kuhusu miradi yenye mguso na matokeo chanya kwa Mazingira na Jamii.

"Utoaji wa hatifungani ya CRDB, utawezesha utekelezaji wa Sera mbalimbali za kitaifa na Malengo Endelevu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa hususan lengo namba saba linalohimiza upatikanaji wa nishati safi kwa wote.

"Kama tunavyofahamu, Serikali imeweka mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa wote ambayo ni rafiki kwa mazingira, hivyo utoaji wa hatifungani hii utawezesha utekelezaji wa malengo na azma ya Serikali ya uwekezaji katika nishati safi, " amesema.

CPA.Mkama amesema utoaji wa hatifungani hiyo utawezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo katika sekta ya umma na binafsi ili kujenga uchumi shindani kwa Maendeleo ya watu.

Pia inawezesha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yaani kwani fedha zitakazo patikana zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo ya jamii, na wananchi watakao wekeza katika hatifungani hii watalipwa riba, hivyo kuinua vipato vyao.

"Utoaji wa hatifungani hii katika fedha mbalimbali za kigeni kutatoa mchango katika jitihada za Serikali za kukabiliana na upungufu wa fedha za kigeni hapa nchini.CMSA imeidhinisha utoaji wa hatifungani ya CRDB kutokana na mazingira wezeshi na shirikishi ya kisera...

" Kisheria na kiutendaji ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi madhubuti wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Uchumi wa kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa imekuwa chachu katika maendeleo na ustawi wa sekta ya fedha, husan masoko ya mitaji, ambapo sasa wanashuhudia uanzishwaji wa bidhaa mpya na bunifu, ikiwa ni pamoja na Multicurrency Green,

Pia Masoko ya mitaji huchochea maendeleo ya uchumi kwa kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha na kuimarisha utawala bora na hivyo kuleta tija kwa kampuni na taasisi.

"Hii inadhihirishwa na mashirika ya Serikali yaliyouza hisa kwa umma na kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam, ambapo kampuni 7 kati ya 10 ambazo ni walipa kodi wakubwa, ni kampuni zilizouza hisa kwa umma na kuorodheshwa DSE.

"CRDB ni miongoni mwa kampuni ambazo zimetumia fursa katika masoko ya mitaji, ambapo mwaka 2009, CMSA ilitoa idhini kwa Benki ya CRDB kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa DSE.Katika mauzo hayo, CRDB ilifanikiwa kupata shilingi bilioni 82.6 sawa na asilimia 439 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 18.8."

Ameongeza kufuatia mafanikio hayo, Benki ya CRDB imeweza kutekeleza Mkakati ulioleta mageuzi na mafanikio yenye tija katika utendaji wa benki kwa wanahisa wake.Bei ya hisa za Benki ya CRDB imeongezeka kutoka shilingi 150 kwa hisa wakati wa mauzo ya hisa ya soko la awali, hadi shilingi 460 kwa hisa, jana tarehe 30 Agosti 2023.

Amefafanua itakumbukwa CRDB ilikuwa ikipata hasara na ilikuwa haitoi gawio kwa Serikali kabla ya kuuza hisa kwa umma na kuorodheshwa DSE. Kutokana na mauzo ya hisa kwa umma na kuorodheshwa DSE, ufanisi wa benki ya CRDB umeongezeka na sasa benki hii inapata faida, inalipa kodi Serikalini na kutoa gawio kwa wanahisa, ikiwa ni pamoja na Serikali.

"Kwa mfano, katika mwaka 2022, CRDB ililipa kodi Serikalini jumla ya shilingi bilioni 337.7 ikiwa ni ongezeko la asilimia 35 kutoka jumla ya kodi ya shilingi bilioni 249.4 iliyolipwa 2021.Pia CRDB ililipa gawio kwa wanahisa Sh. bilioni 94.0...

" Ambapo gawio kwa Serikali lilikuwa shilingi bilioni 32.4, ikiwa ni ongezeko la asilimia 63.6 kutoka gawio la shilingi bilioni 19.8 lililolipwa Serikalini mwaka 2021.CMSA itaendelea kujenga mazingira wezeshi na shirikishi ili kuwezesha taasisi katika sekta ya umma na binafsi kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza miradi."


Mkurugenzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CPA.Nicodemus Mkama akifafanua jambo mbele ya wageni waalikwa mbalimbali  leo Agosti 31, 2023 wakati wa hafla ya uzinduzi wa mauzo ya hatifungani ya CRDB jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana CPA.Nicodemus Mkama akizungumza leo Agosti 31, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mauzo ya hatifungani ya CRDB.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad