Na Karama Kenyunko, Michuzi Blog
MKURUGENZI wa Idara ya Mambo ya Ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amesema wananchi wasisite kutoa taarifa kuhusu vitendo visivyo vya maadili vitakavyofanywa na maofisa wake ili hatua zichukuliwe.
Amesema kuwa mamlaka hiyo haina mchezo na masuala ya maadili hivyo, wasisite kuripoti.
Akizungumza katika maonesho ya Sabasaba leo Julai 3,2021, Haonga amesema TRA ya sasa ni wadau wa wafanyabiashara na sio kama ile ya zamani ambayo walikuwa wanakimbiwa na kuonekana maadui.
Pia ameeleza kwamba ni wakati wa kusaidiana kutoa elimu ya ulipaji kodi na manufaa yake kwa ajili ya nchi hivyo, panapotokea vitendo visivyo vya kimaadili, watoe taarifa.
Haonga amesema kuwa idara hiyo inasimamia masuala yote ya maadili.
Ameongeza kuwa mamlaka hiyo ipo Sabasaba kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na wadau wake kupata huduma.
Haonga ameeleza kuwa serikali imejikita kuboresha huduma mbalimbali katika sekta zote na maboresho hayo hutokana na makusanyo ya kodi.
"Ile kodi ambayo tunaikusanya ndiyo hurudi kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha huduma zetu za kijamii, nitoe wito kwa wadau wetu mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuhakikisha kwamba tunalipa kodi," amesema Haonga.
Ameongeza kuwa ni muhimu kila mwananchi kutekeleza kaulimbiu yao ya kutoa risiti wakati wa kuuza na kudai risiti wakati wa manunuzi ya bidhaa.
"Ukidai risiti unahakikisha kwamba ile kodi inaingia serikalini na kutoa huduma kwa jamii," amesisitiza.
Amesema wanazo huduma nyingi ikiwemo misamaha ya kodi hivyo, wananchi wanaweza kupata maelekezo hatua za kuchukua kupata huduma hiyo.
Pia wanatoa elimu juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwani ndio inayotumika kwa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa elimu hiyo inapaswa kufundishwa hadi shuleni ili wanafunzi wawe na uelewa wa kodi ili iwe rahisi kwao pale wanapokuwa watu wazima walipe kodi bila shinikizo.
No comments:
Post a Comment