PROFESA LIPUMBA MWENYEKITI MPYA TCD - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 3, 2023

PROFESA LIPUMBA MWENYEKITI MPYA TCD

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Mhe. Profesa Ibrahim Lipumba amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) huku makamu wake akiwa ni mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Mhe. Haji Ambar Khamis.

Uchaguzi huo umefanyika leo Julai 3, 2023 katika mkutano mkuu wa TCD uliokuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi wa mwenyekiti mpya ambapo wajumbe kutoka vyama vya Chadema, ACT Wazalendo, CUF, CCM, NCCR Mageuzi na CHAUMMA wakishiriki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji - TCD, Bernadetha Kafuko imesema kuwa Profesa Lipumba amepokea kijiti kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Tanzania Bara, Mhe. Abdulrahman Kinana. Viongozi hao watatumikia uongozi wa TCD kwa kipindi cha mwaka mmoja, kwa mujibu wa Katiba ya TCD. 

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Mhe. Profesa Lipumba amesema vipaumbele vyake katika mwaka mmoja wa uenyekiti wake ni kuongeza ushirikiano na maridhiano ndani ya vyama vya siasa na pia kujenga asasi za kidemokrasia. Pia, mchakato wa kupata katiba uendelee.

“Matumaini yetu ni kwamba kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Kinana ameifanya, sisi tutaiendeleza na tuweze kuwa na kongamano zuri ambalo tunatarajia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi. Kongamano hilo ni jambo ambalo tunaendelea kuwasiliana.” Amesema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad