PURA YASEMA SERIKALI KUENDELEZA GESI ASILIA INAYOPATIKANA KATIKA VITALU - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 6, 2023

PURA YASEMA SERIKALI KUENDELEZA GESI ASILIA INAYOPATIKANA KATIKA VITALU

Na Karama Kenyunko
MAMLAKA ya udhibiti wa mkondo wa juu (PURA) imesema serikali imeamua kuendeleza gesi asilia iliyopatikana katika vitalu vitatu ili kuwa kwenye hali ya kimiminika.

Imesema mkakati huo unalenga gesi hiyo ibebwe kwa wingi kwa ajili ya kwenda kwenye masoko ya nje ikiwemo Japan, Korea na Indonesia.

Akizungumza kwenye maonesho ya Sabasaba leo, Mkurugenzi wa PURA, Mhandisi Charles Sangaweni amesema gesi hiyo ilipatikana katika vitalu vinne lakini inayochakatwa ni kutoka vitalu vitatu.

Amesema kampuni za Shell na Equinor na wabia wenzao ndio waliingia kutafuta gesi hiyo na kwamba baada ya kupatikana kwa makusudi, serikali imeamua kuendeleza gesi hiyo.

Mhandisi Sangaweni ameeleza kuwa gesi asilia hapa nchini imegundulika Songosongo Mnazi Bay huko Mtwara na kwamba walichimba visima 96, vyenye gesi ni 44 na 52 havina kitu.

Ameeleza kuwa wameunganisha gesi hiyo kuleta sokoni kupitia miradi miwili kutoka Songosongo hadi Ubungo kupitia Bomba la nchi 16 na kutoka Mtwara Magimba kwenda Ubungo na Kinyerezi.

"Gesi hiyo inatumika kwenye umeme, viwandani, majumbani na kwenye magari na asilimia zaidi ya 60 ya umeme unaopatikana Tanzania hutokana na gesi hiyo," amefafanua.

Ameeleza kuwa mamlaka hiyo ndio humshauri Waziri wa Nishati kwa masuala yote yanayohusu uendelezaji na utekelezaji wa miradi ya mafuta na gesi kwa mkondo wa juu eneo la kutoa leseni ya uchimbaji, kugawa vitalu kuwapa wawekezaji na kusimamia shughuli zote zinazofanyika wakati wa utafitaji ikiwemo bajeti.

Mhandisi huyo amesema gharama ya kuchimba kisima kimoja kwa nchi kavu ni takribani Dola za Marekani milioni 20 sawa na Sh bilioni 47.

Amesema upande wa bahari kuu, uchimbaji wa visima hivyo hugharimu hadi Dola za Marekani milioni 80 hivyo ni uwekezaji mkubwa unaohitaji kusimamiwa.

Amefafanua kuwa serikali iliingia mikataba yenye hadhi ya Kimataifa kugawana na mwekezaji gharama za utafutaji wa mafuta.

"Wakati wa ugawaji tunaangalia mwekezaji ambaye ameweka fedha zake kutafuta kitu ambacho upatikanaji wake ni 50 kwa 50. Serikali imeangalia kama tutapata zao lolote itatoa mrabaha," amesema.

Amesema serikali hutoa mrabaha kwa gesi inayozalishwa kwa asilimia 100, kwa asilimia 12.5 kwa nchi kavu na baharini hutoa asilimia 7.5.

"Kumekuwa na mikataba hiyo 11 na kati ya hiyo 8 ipo katika utafutaji na 2 ipo kwenye uzalishaji ulioanza tangu mwaka 2004," amesisitiza.
Mkurugenzi wa Pura, Charles Sangaweni akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Pura wakati wa Maonesho ya biashara, Sabasaba jijini Dar es Salaam

Picha ya Pamoja 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad