Waraibu Kunufika na Mikopo ya 10% - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 30, 2023

Waraibu Kunufika na Mikopo ya 10%

 


Na Immaculate Makilika – MAELEZO
SERIKALI imefikia uamuzi wake wa kuongeza kundi la waraibu wa dawa za kulevya katika wanufaika wa mikopo ya fedha zitokanazo na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri nchini ili waweze kufanya shughuli za kujitegemea.

Hayo yamesemwa hivi karibuni bungeni Dodoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kufuatia maelekezo aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akihitimisha katika Kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani, namuelekeza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI azingatie kuongeza kundi la waraibu katika wanufaika wa mikopo hiyo. Kila mkoa uweke mkakati wa haraka wa kuwaratibu waraibu wa dawa za kulevya, kuandaa kanzidata ili kundi hilo muhimu kwa nguvukazi yetu linufaike na mikopo hiyo na liweze kufanya shughuli za kujitegemea”, alieleza Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Alifafanua “Itakumbukwa kuwa, wakati tukiendelea na Bunge hili la bajeti, Serikali ilisitisha kwa muda utoaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 za mapato ya ndani ya halmashauri ili kuweka utaratibu mpya ambao utawezesha Serikali kupata marejesho ya mikopo hiyo kama inavyopaswa. Ili kufanikisha hilo, Serikali iliunda kikosikazi cha wataalamu ili kifanye kazi ya kuandaa mapendekezo ya utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo na urejeshaji wa fedha hizo za mikopo.”

Halikadhalika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alieleza kuwa Kikosikazi hicho kinaendelea kukamilisha taarifa yake ambayo itawezesha Serikali kufanya maamuzi na kuendelea kutoa mikopo kwa makundi mbalimbali. Ambapo taarifa ikishakamilika itawasilishwa ili waheshimiwa wabunge na wananchi wote wapate uelewa kuhusu utaratibu mpya unaoelekezwa na Serikali.

“Nisisitize kuwa lengo la Serikali kutumia benki zetu ni kuongeza ufanisi katika utoaji wa mikopo na urejeshaji ili iendelee kuhudumia walengwa wengine badala ya kuifanya mikopo hiyo itolewe kibiashara”, alisema Mheshimiwa Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad