SACCOS ya JKCI kutoa mkopo wa shilingi milioni 20 - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 22, 2023

SACCOS ya JKCI kutoa mkopo wa shilingi milioni 20

 Na Mwandishi Maalum
MFUKO wa SACCOS ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ina uwezo wa kukopesha wanachama wake hadi kiasi cha shilingi milioni ishirini endapo mwanachama atakidhi vigezo na masharti vilivyowekwa na SACCOS hiyo.

Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa SACCOS hiyo ambaye ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Tulizo shem alipokuwa akizungumza na wanachama wa SACCOS hiyo hivi karibuni wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.

“Sasa hivi SACCOS yetu inauwezo wa kumpa mwanachama wake mkopo wa shilingi milioni ishirini endapo mwanachama huyo hisa zake zinauwezo wa kulipa rejesho la mkopo wake”, alisema Dkt. Shem

Akizungumzia muda wa kupata mkopo Dkt. Shem alisema kwa sasa mwanachama anaweze kupata mkopo ndani ya muda wa nusu saa endapo kama atakamilisha maombi ya mkopo kwa wakati.

“Mwanachama wa JKCI SACCOS anaweza kupata mkopo wake ndani ya dakika thelathini na atalipa marejesho yake ndani ya miezi tisa badala ya miezi sita kama ilivyokuwa hapo awali, tunafanya hivi ili wanachama wetu waweze kufanya maendeleo kupitia mikopo wanayochukua”, alisema Dkt Shem.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mkurugenzi wa Idara ya Tiba ya Moyo Dkt. Tatizo Waane alisema wajumbe wa bodi wa SACCOS ya JKCI wanatakiwa kuangalia fursa mbalimbali zilizopo katika mazingira ya JKCI na kuzitumia kama chanzo cha kutunisha mfuko wa chama kwa kuwekeza katika fursa hizo.

“Wajumbe wa bodi ya SACCOS ya JKCI mnaweza kuwekeza katika usafi na mgahawa huduma zinazotolewa hapa ndani ya JKCI, kama SACCOS itawekeza katika maeneo haya Taasisi itakuwa inailipa Saccos na mapato ya SACCOS yataongezeka”, alisema Dkt. Waane

Dkt. Waane alisema kwa sasa JKCI baada ya kupewa hospitali ya Dar Group idadi ya wafanyakazi imeongezeka hivyo ni wakati sasa viongozi wa SACCOS hiyo kufikisha taarifa kwa wafanyakazi hao ili nao waweze kuwa sehemu ya Saccos hiyo na kunufaika na mikopo inayotolewa.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwani Novemba mwaka jana iliikabidhi JKCI hospitali ya Dar Group hivyo wafanyakazi wa Dar group nao waambiwe umuhimu wa kujiunga na SACCOS hii kuongeza idadi ya wanachama lakini pia kuikuza SACCOS”, alisema Dkt. Waane.

Naye Meneja wa Benki ya NMB tawi la Muhimbili Frank Makungu alisema SACCOS ya JKCI ina muda mfupi lakini inamafanikio makubwa hivyo kuwataka wanachama wa SACCOS hiyo kufuata masharti yaliyowekwa kuifanya SACCOS hiyo kuendelea kuwa katika ubora wake.

“Nimekuwa nikishauriana na viongozi wa SACCOS hii kuhusu mambo mbalimbali, leo nawashauri wanachama mkope kwenye SACCOS yenu, mlipe kwa wakati na muwe mabalozi wazuri wa kuisema vema SACCOS yenu kwa wengine kwani kwakufanya hivyo SACCOS yenu itakuwa”, alisema Makungu.

Akizungumzia uzoefu alionao katika vyama vya mikopo Afisa Ushirika Ofisi ya Msajili Msaidizi Olivia Kaiza alisema SACCOS nyingi zinashindwa kuendelea kwa sababu ya kutegemea posho katika kukata mapato ya Mfuko hivyo kuitaka JKCI kuhusisha mishahara kulipa mkopo kuliko kutegemea posho.

“Posho ni fedha ya ziada ambayo inaweza kusitishwa wakati wowote, nawashauri wajumbe wa bodi ya JKCI SACCOS kutotegemea posho kukata riba za mikopo bali mikopo ikatwe kwenye mishahara maana mshahara ni lazima mtu apate”, alisema Oliva.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad