HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 24, 2023

Watuhumiwa 12 washikiliwa kwa kufanya vurugu zilizopelekea kifo cha mtu mmoja

 

JESHI la Polisi mkoani Arusha linawashikilia watuhumiwa 12 kwa tuhuma za kufanya vurugu pamoja na uharibifu wa vitu mbalimbali na kupelekea mtu mmoja kufariki dunia.

Akitoa taarifa hiyo leo Mei 22, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo amesema mei 22, 2023 muda wa saa 5:40 asubuhi huko katika Kitongoji cha Magomeni kijiji cha Jangwani eneo la Mto wa Mbu Wilaya ya Monduli Mkoa wa Arusha, Askari wa hifadhi ya Manyara wakiwa katika doria ya kawaida eneo la ziwa Manyara walikamata Wavuvi watatu waliokuwa wakivua samaki katika maeneo yaliyozuiliwa kwa uhifadhi.

ACP Masejo amebainisha kuwa mara baada ya kukamatwa kwa wavuvi hayo, walijitokeza wavuvi wengine na kuzusha vurugu iliyopelekea askari hao wa uhifadhi kushindwa kuwachukua watuhumiwa hao na kwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi.

Kamanda Masejo ameendelea kufafanua kuwa umati wa watu hao walikwenda hadi kwenye ofisi ya kijiji cha Jangwani na kufanya uharibifu mkubwa katika ofisi hiyo ya serikali kwa kuvunja madirisha pamoja na kuchana bendera ya Taifa na kuondoka nayo kwa madai kuwa wavuvi wenzao wamezamishwa maji wakati wanakamatwa na Askari wa uhifadhi.

Aidha baada ya uharibifu huo, kundi hilo liliamua kuelekea ofisi na makazi ya Askari wa TANAPA yaliyopo Mto wa Mbu, lakini wakati wakiwa njiani walivamia ofisi na makazi ya Askari wa TANAPA na kufanya uharibifu mkubwa wa magari kwa kutumia marungu na mawe pamoja na kupanga mawe barabarani kuzuia watumiaji wengine wa barabara wasiendelee na shughuli zao.

ACP Masejo amebainisha kuwa licha ya juhudi za kuwazuia kuingia katika ofisi na makazi hayo ya Askari wa TANAPA watu hao waliendelea kupambana na askari wa uhifadhi na ndipo jeshi la Polisi waliongeza nguvu kuokoa na kuzuia madhara zaidi kwa binadamu na mali za watu binafsi na za serikali.

Aliendelea kueleza kuwa kutokana na ghasia hizo mtu mmoja alipoteza maisha na watu wengine saba walijeruhiwa na wamelazwa hospitali wakiendelea na matibabu.

ACP Masejo amesema upelelezi wa shauri hilo unaendelea ili kubaini walioanzisha na kushiriki katika vurugu hizo pamoja na kuchunguza madai ya wananchi kuhusiana na wavuvi waliozamishwa katika maji.

Sambamba na hilo uchunguzi ukibaini ukweli kulingana na ushahidi watu hao watafikishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linatoa onyo kali kwa baadhi ya watu ambao wanatabia ya kupambana na vyombo vya dola ambao kimsingi wamepewa dhamana ya kulinda maisha ya watu, mali zao pamoja usalama wa nchi kwani inaweza kusababisha madhara makubwa.

Lakini pia jeshi hilo limesema endapo kuna changamoto yoyote zipo taratibu nzuri za kufuata kuliko kufanya vurugu na kujichukukulia sheria mikononi kwa kupambana na vyombo vilivyopewa mamlaka kisheria ya kulinda maisha ya watu, mali zao na rasilimali za Taifa

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad