HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 19, 2023

JAMII YAHIMIZWA KUFANYA MAZOEZI KWA AFYA BORA

  Na Fauzia Mussa Maelezo

JAMII imeshauriwa kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo kila siku ili kuondoa takataka zisizohitajika ambazo zinasababisha maradhi mbalimbali mwilini.

Daktari dhamana Wilaya ya Kaskazini "B" Maryam Hamdu Khalfan ameyasema hayo alipokuwa akitoa elimu ya Afya juu ya maradhi yasioambukiza kwa wanakikundi cha wagonjwa wa maradhi hayo wakati wakipatiwa huduma za Afya katika ngazi ya jamii huko Bumbwini Makoba Wilaya ya Kaskazini "B"

Alifahamisha kuwa kutokufanya mazoezi kunapelekea mafuta kukaa na kuganda kwenye mishipa ya damu jambo ambalo linaifanya mishipa hiyo Kuwa dhaifu na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi hivyo ameishauri jamii kufanya mazowezi angalau nusu saa kwa siku ili kusaidia kuyeyusha mafuta hayo.

Aidha alifahamisha kuwa endapo mafuta yataganda katika mishipa ya damu kunasababisha maradhi ya sindikizo la juu la damu (presha) na hatimae kupelekea mtu kupata kiaharusi (stroke) maradhi ambayo yanapelekea ulemavu wa daima.

Alielezea kuwa kufanya mazoezi mara kwa mara licha ya kuuchangamsha mwili na kuuweka katika hali ya uimara pia ni njia moja wapo ya kujikinga na maradhi hayo hivyo amesisitiza jamii kutokuwacha kufanya mazoezi ili kuboresha afya zao.

"Jamii haina Utamaduni wa kufanya mazoezi tukidhani mazoezi ni kukimbia au kubeba vyuma kumbe hata kutembea kwa dakika 30 tu kunatosha kuwa wewe umefanya mazoezi " Alisema Dkt. Maryam
Aidha Dkt.Maryam aliitaka jamii kupendelea kunywa maji ya moto ya limau kabla ya kula chochote kwani kinywaji hicho kinarahisisha mzunguko wa damu na kuyeyusha mafuta mwilini.

"Unywaji wa maji Moto yaliyochanganywa na kipande cha limau kunasaidia mzunguko wa damu na kufanya jasho litoke kwa wingi mwilini, tujenge mazowea ya kutumia maji haya ili tusafishe miili yetu kwa kutoa jasho jingi na kuisaidia mishipa ya damu kufanya zake yake." Dkt. Maryam alishauri
Hata hivyo dkt. Maryam aliwashauri wanakikundi hao kushirikiana na wahaudumu wa afya wa kujitolea katika jamii (CHV) kuandaa utaratibu maalum wa kukutana na kufanya mazowezi ili kupunguza msongo wa mawazo unaohatarisha afya zao.

Nae Daktari dhamana kituo cha Afya Bumbwini Misufini Aisha Ali amewaomba wanakikundi hao kuwa na mashirikiano mazuri na kufuatilia huduma hizo Kila ifikapo tarehe waliopangiwa na kuwataka kutoa taarifa za dharura kwa madaktari pindi wanaapofikwa na tatizo kabla ya tarehe yao ya kliniki kufika.

Kwaupande wao wanakikundi hao wameishukuru Wizara ya Afya kwa kushirikiana na PharmaAccess International kuwasogezea huduma za Afya karibu na jamii na kuahidi kuitumia vyema fursa hiyo yenye lengo la kuboresha huduma za Afya Nchini.

Itakumbukwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amekua akiwasisitiza wananchi kufanya mazoezi kila siku ikiiaminika kuwa kunaboresha Afya zao na kuwakinga na maradhi.
Daktari dhmana Wilaya ya Kaskazini “B” Maryam Hamdu Khalfan akizungumza na wanakikundi cha maradhi yasioambukiza alipokuwa akiwapatia elimu ya maradhi hayo wakati wa zoezi la utoaji wa huduma za Afya katika ngazi ya jamii huko Bumbwini Makoba Mkoa wa Kaskazini Unguja. 
Afisa mradi wa kuwafikia wagonjwa wa maradhi yasioambukiza kutoka PharmAccess International Queen – Ruth Msina akimsaidia mzee kuingia katika chumba cha daktari wakati wa zoezi la utoaji wa huduma za Afya katika ngazi ya jamii kwa wagonjwa wa maradhi hayo huko Bumbwini Makoba Wilaya ya Kaskazini “B” . 
PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad