HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 12, 2023

Kilimanjaro Marathon yamlilia John Bayo

 

KILIMANJARO Marathon Company Limited imeelezea kuhuzunishwa kufuatia kifo cha Mkurugenzi wa mbio maarufu ya Kilimanjaro International Marathon, Bwana John Bayo ambaye alifariki Jumanne asubuhi Jijini Arusha.

Taarifa iliyotolewa na waandaaji wa Kilimanjaro International Marathon imemuelezea marehemu Bayo kama mtu mwema na moja ya mihimili mikuu ya Kilimanjaro Marathon ambayo ni mbio kubwa kuliko zote Tanzania.

KMCL, kupitia taarifa hiyo imetuma salamu za rambirambi kwa familia yake marehemu Bayo, ndugu, jamaa, marafiki na kwa wadau wote wa riadha ndani na nje ya Tanzania.

“Mtu mwema kiasi hiki anapofariki, inakuwa vigumu sana kuzungumza kwani tumepoteza muhimili mkubwa mno katika Kilimanjaro Marathon na rafiki wa kipekee,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa waandaaji hao, Bw. Bayo alikuwa mmoja wa waanzilishi wa mbio hiyo ya Kilimanjaro Marathon mwaka 2003 ambapo washiriki wasiozidi 500 walikimbia mbio za kujifurahisha tu lakini zaidi ya miaka 20 baadaye, mbio hiyo sasa inawavutia zaidi ya washiriki 12,000 kutoka nchi zaidi ya 55 duniani.

Bayo alikuwa mchapa kazi hodari ambaye alitumia ujuzi wake wote na uzoefu katika Kilimanjaro Marathon hadi umauti unamchukua.

“Alishirikiana pia na waandaaji wa mbio nyingine nchini Tanzania na kuwafundisha namna ya kuandaa mbio kwa weledi,” walisema waandaaji hao.

Waandaaji hao waliendelea kusema kuwa Bw. Bayo, katika uhai wake aliwahimiza wakimbiaji wengi wa kitanzania kushiriki katika mbio mbalimbali nje ya nchi.

“Kwetu sisi alikuwa kama ndugu, mstaarabu na hodari katika kazi yake ambayo aliifanya kwa weledi mkubwa, tutamkumbuka mno,” walisema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad