HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 17, 2023

WALEZI WA WATOTO KUPIKWA KWA MTAALA MMOJA- KAMISHNA MSAIDIZI MAKONA

 

Na WMJJWM, DODOMA
SERIKALI ipo mbioni kukamilisha Mwongozo wa Mafunzo wa Malezi ya Watoto wadogo na wachanga ili kuleta uwiano na uelewa unaofanana wa ufundishaji wa Malezi na Makuzi kwa nchi nzima.

Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Baraka Makona ameyasema hayo

alipomuwakilisha Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando wakati wa kufunga mafunzo ya wiki mbili ya Walezi wa Watoto wadogo Mkoa wa Dodoma ambapo jumla ya Wahitimu 155 wamefuzu mafunzo hayo yaliyofanyika shule ya sekondari ya Dodoma.

Makona amesema Serikali ilizindua Mwongozo wa Malezi mwaka 2022 mwezi Septemba ili kuweka usawa wa mtaala ambao utatumika kulea watoto kwa kipindi wakacho kuwa kwenye vituo ambao bado haujaanza kutumika rasmi.

"Mwongozo tumeuzindua mwaka jana mwezi Septemba na kilichobaki ni kuwakabidhi nyinyi, nimewaagiza waratibu wauingize katika utaratibu wa mafunzo kwa mikoa mingine" amesema Makona

Makona amebainisha kuwa, katika kuboresha utoaji wa huduma za malezi kwenye vituo vya kulelea watoto wadogo na mchana, Wizara imetoa mafunzo kazini kwa wamiliki wa vituo na walezi wa watoto nchini kwa kuhakikisha wanakuwa na Mtaala mmoja.

"Tunatambua kulikuwa na tatizo la kila Chuo kuwa na Mtaaala wake, lakini sasa hivi, tumefanikiwa kuviratibu na kuviweka vyuo vyote kwenye utaratibu mmoja na Shabaha yetu ni kuwa na mtaala mmoja lakini pia Mtihani mmoja wakuwapima kwa nchi nzima" amesema Makona.

Katika hatua nyingine, Kamishna Msadizi wa Ustawi wa Jamii Makona amewataka wahitimu hao kuwa na ushirikiano na viongozi waliopo kwenye maeneo yao kwa kutoa taarifa za changamoto zinazowakabili huku akichagiza umuhimu wa kuwepo kwa vyama vya uongozi miongoni mwao.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI ambaye pia ni Mratibu Mwandamizi wa mafunzo ya Malezi Bw. Chris Maduhu, amesema kuna mabadiliko yanayojitokeza kila wakati kwa walezi wasiokua na sifa na wanazidi kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki ya uwasilishaji taarifa ili waweze kuwafikia watoa huduma wote ambao hawana elimu stahiki ya malezi.

"Mafunzo ya awamu ya kwanza yaliwafikia walezi 80 mwaka 2019, 124 kwa mwaka 2021 na 155 mwaka huu 2023, mafunzo haya yameenda kuwa chachu ya kujenga mahusiano mazuri kati ya watoa huduma na maafisa na kuongeza usajili wa vituo kwa kuelewa na kuzingatia Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009"

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw Tito Lulandala amesema ni wakati wa wazazi na wanajamii kusema na watoto juu ya hatari zilizopo huko nje sio kwa kuwazidishia adhabu bali kwa kuwaambia hatari wanazoweza kukutana nazo.

"Sisi jukumu letu kubwa ni kusimamia maadili kwa misingi ya utamaduni wa Mtanzania, mojawapo wa jambo tunalofanya ni kuhamasisha wadau wa makuzi na malezi ya watoto kufanya malezi bora yanayozingatia maadili ya msingi wa utamaduni wa mtanzania kwa kuzingatia Sheria zote na nyenzo zote za kisera na mwongozo wa malezi ambao umetolewa kwa waraka wa elimu namba 6 mwaka 2020" amesema Lulandala.

Naye Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Matibu Salum, akiwaapisha wahitimu hao amewataka walimu kutoa ushirikiano pale wanapoona wamiliki wa vituo ama wenzao wanafanya vitendo vya uvunjifu wa haki ya Mtoto kwani kufanya hivyo ni kosa na sheria haitasita kuchukua mkondo wake.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad