HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 31, 2023

SERIKALI ya Zanzibar Imedhamiria Kupeleka Usawa wa Maendeleo kisiwani Pemba

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza dhamira yake ya kupeleka usawa wa maendeleo kisiwani Pemba katika nyanja zote ikiwemo kuimarisha miundombinu ya barabara na ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar, Ikulu Zanzibar.

Dk. Mwinyi, alieleza Serikali imedhamiria kuifungua Pemba zaidi kwa maendeleo makubwa mara tu baada ya kukamilika kwa ujenzi mpya wa uwanja wa ndege wa kimataifa ili kuweka uwiano sawa na mandhari ya kisiwa cha Unguja kwa uondoa utofauti wa maendeleo uliopo baina yao.

“Ki maendeleo Unguja na Pemba hazipo sawa, tunataka kuibadilisha Pemba kuwa sawa na Unguja kimaendelo” aliahidi Dk. Mwinyi.

Alisema ujenzi wa barabara kutoka Chake hadi Mkoani na Ujenzi wa uwanja wa ndege mpya kwa sasa ni miradi mikubwa ya maendeleo kisiwani humo ambayo ni muhimu sana kwa Zanzibar.

Dk. Mwinyi alisema tayari Serikali imefikia hatua nzuri ya mazungumzo baina yao wakandarasi wa ujenzi huo na kueleza tayari mchakato wa awali wa ujenzi wa jengo la taminali kwa uwanja wa ndege umeanza.

Alisema kukamikika kwa miradi hiyo kutaifungua zaidi Pemba kimaendeleo kwa kuruhusu ndege kubwa za kimataifa kutua kisiwani humo.

Naye Balozi Concer alieleza dhamira ya Uingereza kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ushirikiano wao wa miradi hiyo ya Pemba, alisema mchakato wa fedha upo tayari kutoka kwa hazina kuu ya Uingereza na kusisitiza matarajio yake ya kuanza haraka kwa ujenzi huo.

Aidha, Balozi Concer alimuahidi Rais Mwinyi kwamba Serikali ya Uingereza na Zanzibar wataendeleza ushirikiano uliopo katika kukuza Sekta za maendeleo na kuimarisha uhusiano wao kidipolomaisia uliopo baina yao.

Uhusiano wa diplomasia baina ya Tanzania na Uingereza ni wa kihistoria, ambao umeimarika zaidi kwenye sekta za biashara, kilimo, madini na viwanda na kutajwa kuwa Uingereza ni mwekezaji mkubwa wa kigeni kwenye sekta hizo.

Tanzania ikiwa mwanachama wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth) pia ni mshirika mzuri na Uingereza tokea mwaka 1964, kwasasa ina balozi wake Dar es Salaam, David Concar tangu mwaka 2020 na Tanzania balozi wake nchini Uingereza ni Dk. Asha Rose Migiro. Mataifa mawili yameendelea kuimarisha uhusiano baina yao kwa fursa nyingi za maendeleo kupatikana pande mbili hizo ikiwemo Zanzibar.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad