HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, December 11, 2022

TTCL YAPELEKA INTANET KWA WAPANDA MLIMA WA KILIMANJARO

Waziri Nape akiangalia njia ya kuelekea kileleni cha Mlima Kilimanjaro mara baada ya hafla ya kuelekea Uzinduzi wa Huduma ya Intaneti katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro iliyofanyika Marangu Gate Mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (wa pili kulia waliosimama) akishuhudia Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA) pamoja na Shirika la TTCL wakisaini Hati ya Makubaliano(MoU) ya ushirikiano katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Kulia wanaosaini ni Kamishna Mhifadhi Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Emilian Kihwele na Mkurugenzi Mkuu Shirika la Mawasiliano Tanzania, Mhandisi Peter Ulanga (kushoto).
Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Wahandisi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL (waliosimama) waliofanikisha ujenzi wa miundombinu ya Mawasiliano mpaka Kilele cha Mlima Kilimanjaro, mara baada ya hafla ya kuelekea Uzinduzi wa Huduma ya Intaneti katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro iliyofanyika Marangu Gate Mkoani Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakutugenzi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL, Bi Zuhura Snare Muro akizungumzia jinsi Bodi yake itakavyoendelea kuleta mageuzi katika sekta ya Mawasiliano nchini wakati wa hafla ya kuelekea Uzinduzi wa Huduma ya Intaneti katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro iliyofanyika Marangu Gate Mkoani Kilimanjaro.
Waziri Nape akifungua kitambaa kuangalia njia ya kuelekea kileleni cha Mlima Kilimanjaro mara baada ya hafla ya kuelekea Uzinduzi wa Huduma ya Intaneti katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro iliyofanyika Marangu Gate mkoani Kilimanjaro.

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) limefanikiwa kufikisha huduma za mawasiliano ya Intaneti kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro, ikiwa ni juhudi za kuunga mkono Serikali kutangaza vivutio vya utalii nchini.

Akizungumza katika hafla ya awali kuelekea uzinduzi wa mawasiliano ya Data Katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro uliofanyika Makao Makuu ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ameipongeza TTCL kufanikisha mradi huo wa kuweka mawasiliano katika Mlima Kilimanjaro.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kusimika huduma za mawasiliano katika kilele cha Mlima kilimanjaro, jambo ambalo litaongeza kasi ya kuutangaza mlima huo duniani na kuvutia idadi kubwa ya watalii kuutembelea.

"Leo ni siku muhimu kwa Shirika letu la TTCL na Tanzania tunapokwenda kushuhudia tukio la kihistoria la uzinduzi wa intaneti katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, utakaofanyika pia rasmi kwenye kileleni cha mlima Desemba 13, 2022 tukiwa huko kileleni," alisema Mhe. Nnauye.

Jumla ya kilometa 44.7 za njia ya Mkongo wa Mawasiliano zimejengwa kuanzia Kituo cha Marangu hadi kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, uwekezaji ambao umefanikisha vituo vyote vilivyopo katika Mlima Kilimanjaro kupata mawasiliano ya intaneti na simu za mezani.

"Tangu kuzinduliwa kwa huduma za mawasiliano katika vituo vya awali, watalii wanaopanda mlimani wameanza kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki wakiwa mlimani na kuelezea uzuri wa vivutio vyetu jambo ambalo linaendelea kuutangaza utalii nchini, licha ya kurahisisha shughuli za huduma kwa watalii zinazofanywa na taasisi mbalimbali katika Mlima Kilimanjaro," alisisitiza Waziri Nnauye.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Eng. Peter Ulanga alisema uwepo wa huduma hiyo ya mawasiliano katika Mlima Kilimanjaro itaboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa watalii mlimani, pia wanapopata dharura yoyote wakiwa safarini.

Aidha aliongeza uwepo wa huduma za mawasiliano utaimarisha shughuli za ulinzi na usalama kwa watalii wakiwa mlimani kupitia mamlaka husika jambo ambalo ni kivutio cha kuchocheza na kuvutia watalii wengi kuutembelea.

"Mkakati wa Shirika wa miaka mitano ni kuhakikisha huduma za mkongo zinawafikia wananchi katika makazi yao, maeneo ya biashara, maofisini na sehemu za vivutio vya utalii wetu, TTCL inatambua umuhimu wa utalii nchini hivyo tutaongeza nguvu kutoa huduma za mawasiliano kupitia mkongo katika maeneo mengine ya utalii ili kuchochea shughuli za utalii nchini," alibainisha Eng. Ulanga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad