HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 23, 2022

TPA NA TRC YAANZA KUTEKELEZA MAELEKEZO YA MAKAMU WA RAIS BANDARI YA TANGA

 


Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA) na Shirika la Reli Nchini (TRC) imeanza mara moja ukarabati na urejeshwaji wa reli inayoanzia stesheni ya reli Tanga kuelekea Bandarini jijini humo ili kuhakikisha mzigo unashushwa bandari hapo na kuwafikia walaji kwa wakati.

Kazi hiyo imefanywa siku moja baada ya maelekezo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Philip Mpango kuelekeza TPA na TRC kukarabati na kurejesha reli inayotoka stesheni ya treni Tanga kuelekea Bandarini wakati alipotembelea mradi wa upanuzi wa Bandari ya Tanga.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya kazi hiyo Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema Serikali itaendeleea kutekeleza maelekezo na mipango yake katika miradi mbalimbali ili kuhakikisha malengo iliyojiwekea yanatimia kwa wakati.

“Niwapongeze sana TRC na TPA kwa uharaka wa kutekeleza maelekezo ya viongozi, na hii iwe kianzio kwa wataalaam kufanya kazi zao kwa wakati maana nimeona hapa tayari mmeanza kazi na muhakikishe inakamilika ndani ya muda mfupi na treni inaanza kutoa huduma bandarini’ amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amewataka TRC na TPA kushirikiana kwenye utendaji kwani ufanisi wa utendaji unategemea baina ya taasisi hizo na kuwasisitiza kuwa na vikao vya mara kwa mara ili kumaliza changamoto mbalimbali za huduma zilizopo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uendeshaji kutoka TRC, Focus Sahani, amemuhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa kazi hiyo itakamilika ndani ya wiki mbili na treni kuanza majaribio ili kupima mapungufu yaliyopo na kuyarekebisha kabla ya kuhudumia mizigo bandarini.

Kaimu Mkurugenzi Sahani ameongeza Shirika linaendelea na ukarabati wa mabehewa ili kuhakikisha mzigo unaopitia bandarini unahudumiwa kwa wakati na kuongeza ufanisi katika usafirishaji wa mizigo baina ya Mkoa huo na mikoa ya karibu.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete akiangalia miundombinu ya reli ya kutoka Stesheni ya Tanga kwenda Bandari ya Tanga, wakati alipokagua utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ya kuikarabati reli hiyo na kurudisha vipande vilivyotolewa wakati alipokagua maendeleo ya mradi wa bandari ya Tanga.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) Focus Sahani kuhusu maendeleo ya Ukarabati wa reli ya kutoka Stesheni ya Tanga kuelekea Bandarini, jijini Tanga.

Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ukarabati wa reli ya kutoka Stesheni ya Tanga kuelekea Bandarini, jijini Tanga. Ukarabati huo umeanza kufanyika baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango kuelekeza Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA) kurejesha huduma za reli bandarini hapo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad