Na Muhidin Amri, Nyasa
WAKALA wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) imesema,kuanzia sasa itaanza kuwatumia baadhi ya vijana wanaomaliza elimu ya kidato cha nne waliopata ujuzi katika vyuo vya ufundi(Veta) ili kusimamia na kuendeleza miradi ya maji nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegilo,alipotembelea na kukagua mradi wa maji unaotekelezwa katika kijiji cha Liuli wilayani Nyasa pamoja na kuzungumza na viongozi wa jumuiya ya watumia maji.
Alisema,katika mpango huo Ruwasa itashirikiana na serikali za vijiji kuwapata vijana hao na kuwapeleka kwenye vyuo vya ufundi stadi(Veta)ili wakapate ujuzi kabla ya kupewa jukumu la kuendesha miradi ya maji ambayo inahitaji watu wenye ujuzi na waadilifu.
Aliongeza kuwa,hatua hiyo itasaidia kupata vijana wenye ujuzi katika kusimamia na kufanya matengenezo pindi miradi inapoharibika,badala ya kuwatumia watu wasio na ujuzi kusimamia na kuendesha miradi ya maji.
Aidha,amewataka wananchi kuvuta maji kwenye nyumba zao ili kutimiza adhima na lengo la serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani,badala ya kukusanyika kwenye vituo vya kuchotea maji.
Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Rebman Ganshonga alieleza kuwa,mradi wa maji Liuli ni kati ya miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa katika wilaya ya Nyasa na kampuni ya Emirate Co Ltd.
Alisema,kazi kubwa katika ujenzi wa mradi huo ni kujenga matenki matatu,kujenga chanzo cha maji na kulaza mabomba umbali wa km 50 na hadi sasa ujenzi wake unaendelea vizuri.
Naye Meneja mradi Jeremiha Maduhu alieleza kuwa,mradi huo ulianza kujengwa Mwezi Aprili 2022 na unatarajiwa kukamilika mwezi April 2023 ambapo utahudumia vijiji saba vyenye jumla ya wakazi 14,186.
Maduhu alitaja gharama za mradi ni Sh. Bilioni 6,595,019,723 na kiasi cha fedha zilizotolewa ni Sh.milioni 989,252,958.50 na hadi sasa kazi zilizofanyika ni ujenzi wa chanzo,ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji la lita laki tano,ununuzi wa mabomba na ujenzi wa vituo ishirini na nne vya kuchotea maji.
Mwenyekiti wa kijiji cha Liuli Menas Chale,ameishukuru wizara ya maji kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kwa kujenga mradi huo ambao utamaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika kijiji hicho na vijiji vya jirani.
Chale amehaidi kuwa,serikali ya kijiji itahakikisha miundombinu ya mradi huo inalindwa na kutumia maji kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Hata hivyo,amemuomba mkandarasi wa mradi huo kujenga vituo vya kuchotea maji karibu na makazi ya wananchi ili iwe rahisi watu kupata huduma ya maji katika makazi yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegilo aliyeshika fimbo,akiangalia mchoro wa mardi wa maji unaojengwa katika kijiji cha Liuli wilayani Nyasa kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 6,katikati Meneja mradi Jeremiha Maduhu.
Meneja mradi wa maji na Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nyasa Jeremiha Maduhu kushoto,akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji unaotekelezwa katika kijiji cha Liuli kwa Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegilo katikati na Meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Rebman Ganshonga.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegilo akikagua ubora wa tenki la kuhifadhi maji katika kijiji cha Liuli alipokuwa katika ziara ya kutembelea miradi ya maji inayotekelezwa katika vijiji mbalimbali wilayani Nyasa.
Meneja Ufundi wa Kampuni ya Emirate Builder Company Ltd inayojenga mradi wa maji katika kijiji cha Liuli wilaya ya Nyasa Said Msangi kushoto,akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) Mhandisi Clement Kivegilo aliyetembelea mradi huo.
No comments:
Post a Comment