HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 26, 2022

Benki ya Maendeleo TIB yahamasisha miradi ya maendeleo Wiki ya Huduma za Fedha


 Baadhi ya wakuu wa wilaya waliotembelea Banda la Benki ya Maendeleo TIB kwenye maonesho ya Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza. Wapili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Busega mkoani Simiyu, Gabriel Zakaria, Mkuu wa wilaya ya Butiama, Mwalimu Moses Kaegele (watatu kulia), Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapawa (katikati) na Mkuu wa wilaya Tarime, Kanali Michael Mtenjele (watatu kushoto). Wengine ni maafisa wa Benki ya Maendeleo TIB.  
 
Na Mwandishi Wetu,         

Benki ya Maendeleo TIB imehamasisha umma kuchangamka fursa za mikopo zinazotolewa na benki hiyo ili kuwekeza katika miradi ya maendeleo kwa ajili kuchagiza ukuaji wa uchumi nchini.

Wito huo umetolewa na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Benki ya Maendeleo TIB, Bi. Giusy Mbolile kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza.

Bi. Mbolile amesema kuwa Benki ya Maendeleo TIB ina wajibu wa kuwezesha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na wa kati kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi hapa nchini hivyo amewasihi wawekezaji wenye miradi ya kimkakati kuitumia benki hiyo ili kufanikisha miradi hiyo.

“Benki ya Maendeleo TIB ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa malengo ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na wa kati kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, hivyo nawasihi wawekezaji wenye miradi ya kimkakati kuitumia benki ili kufanikisha uwekezaji huo,” alisema.

Aliongeza kuwa benki hiyo inatoa mikopo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, madini, huduma, miundombinu, nishati na maji pamoja na programu za mikopo ya wawekezaji wadogo na wakati (SMES). 

Ameongeza kuwa mikopo hiyo inatolewa ili kuchagiza ukuaji wa shughuli za kiuchumi ili kutekeleza mipango mbali mbali ya Serikali inayolenga Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu hapa nchini.

“Mikopo yetu ikiwemo ya Sekta ya viwanda inalenga kuleta kusaidia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwa lengo la Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu hapa nchini,” aliongeza.

Aliongeza kuwa benki imetumia maadhimisho hayo kwa ajili ya kusambaza taarifa na kujua mitazamo, kero na mahitaji ya taarifa za wadau wa benki hiyo ili kuiwezesha kuimarisha bidhaa na huduma zake.  

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21 – 2029/30 kupitia elimu kwa umma.  

Kwa mwaka huu maonesho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yameanza tarehe 21 Novemba na yanatarajia kufikia tamati tarehe 26 Novemba jijini Mwanza yakiwa na kauli mbiu “Elimu ya Fedha kwa Maendeleo ya Watu.” 
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe. Veronica Kessy (kulia) akizungumza na baadhi ya maofisa wa Benki ya Maendeleo TIB kwenye maonesho ya Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza. Kushoto ni Afisa Biashara Mwandimizi, Bw. John Mboje na Afisa Uhusiano Mwandamizi, Bi Giusy Mbolile (kulia). 
Kamishna Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema (kushoto) akikabidhiwa zawadi na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Benki ya Maendeleo TIB, Bi Giusy Mbolile (kulia) wakati alipotembelea Banda la Benki ya Maendeleo TIB kwenye maonesho ya Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad