HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 3, 2022

Makamu wa Pili akifungua maduka Kisiwandui

 Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar wametakiwa kuwa mfano katika kuhamasisha ulipaji wa Mapato kwa Wafanyabiashara ili kuongeza uelewa kwa Wananchi katika suala hilo.


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito huo katika Hotuba iliyosomwa kwa Niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla katika ufunguzi wa jengo la maduka ya biashara afisi kuu ya ccm kisiwandui Zanzibar .

Ameeleza kuwa kukamilika kwa Maduka hayo kutatoa fursa kwa Wafanyabiashara na Wajasiriamali kuwa na eneo la kisasa la kufanyia Biashara zao ambalo litasaidia kuongeza mapato kupitia Wafanyabiashara hao.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa ni jambo la kupongezwa kwa Chama Cha Mapinduzi kujenga Maduka hayo hatua ambayo itasaidia kuongeza kipato kwa Chama ili kupunguza ruzuku pamoja na michango ya wahisani ili kuendesha vyema shughuli mbali mbali za Chama.

Sambamba na hayo Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa katika mradi huo kutazalika ajira zitakazosaidia kufikia Azma ya Serikali ya Awamu ya Nane kuzalisha ajira zaidi ya Laki Tatu (300,000) ndani ya muda wa miaka mitano (05).

Aidha ameeleza kuwa juhudi za Wafanyabiashara na Taasisi Binafsi zinasaidia Serikali katika kuwapatia ajira wazanzibari ili kuweza kujipatia kipato cha kila siku.

Pamoja na mambo mengine Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa amekemea tabia ya baadhi ya Wafanyabiashara wanaokodishwa maduka na baadae kukodisha wengine kwa bei ya juu na kueleza kuwa wafanyabiashara aina hiyo wachukuliwe hatua stahiki ikiwemo kufutiwa mikataba na kufikishwa katika vyombo vya Sheria.

Mhe. Dkt. Mwinyi amewaasa Wafanyabiashara watakaobahatika kupata maduka hayo kutunza usafi wa maeneo yaliyowazunguka ili kuweka mji safi pamoja na kukusanya taka katika maeneo husika.

Nae Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Maalim Kombo Hassan Juma Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ameeleza kuwa ujenzi wa Maduka hayo ni kusimamia Azma ya Chama Cha Mapinduzi kuweza kuongeza vyanzo vya Uchumi ndani ya Chama hicho na kupunguza utegemezi kwa wadau mbali mbali.

Aidha Maalim Kombo ameeleza kuwa maduka hayo mbali na kupendezesha Mji Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kimejipanga zaidi kujenga ghorofa ili kuendana na kasi ya majengo mazuri na yenye kukidhi vigezo.

Akisoma Taarifa ya Ujenzi huo Katibu wa Kamati Maalum Uchumi na Fedha Ndg. Afadhali Taibu Afadhali ameeleza kuwa Ujenzi wa Maduka ya Afisi Kuu ya CCM Zanzibar umejumuisha maduka Arobaini na Saba (47), Vyoo na mashine tatu (03) za kutolea pesa (ATM MACHINE) na kueleza kuwa hatua hiyo ni kuunga Mkono utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi mwaka 2020-2025 ambapo kukamilika kwake kutaweza kutoa ajira zaidi ya Mia Moja (100).

Ameeleza kuwa Afisi Kuu ya CCM Zanzibar wanaunga Mkono na kuthibitisha uwajibikaji wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kusimamia Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa vitendo jambo ambalo linawapa moyo Wananchi wa Zanzibar.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiweka Jiwe la Msingi la Jengo la Maduka ya Biashara Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar kwa Niaba ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Zanzibar ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kuaishiria ufunguzi wa Jengo la Maduka ya Biashara Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar kwa Niaba ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein ali mwinyi.
 Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdullah akizungumza na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na Wafanyabiashara katika ufunguzi wa Jengo la Maduka ya Biashara Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar ambapo amewataka Wafanyabiashara kutunza maduka hayo na kuyaweka katika hali ya usafi.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar na Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Taifa Maalim Kombo Hassan Juma akizungumza machache katika hafla ya ufunguzi wa Jengo la Maduka ya Biashara Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad