HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 21, 2022

Wazee CCM wawataka wastaafu kumuunga mkono Rais Mwinyi

 

 Na Mwandishi Wetu, Unguja

MWENYEKITI Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Mjini na Magharibi Unguja, Bw Boraafya Sirima Juma amewataka viongozi wastaafu ndani ya chama kuunga mkono juhudi na hatua mbalimbali zinazochukiliwa  na  Rais Hussein Ali Mwinyi katika kuleta mageuzi ya kiuchumi na kuinua maisha ya wazanzibari wote.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Bw Juma ya kutoa wito kwa waastaa amekemea pia vitendo vya baadhi ya wastaafu ndani ya CCM kuwa kikwazo viongozi waliopo kutekeleza majukumu yao. 

“Kustaafu siyo dhambi ni zuri na lipo kisheria. Wapo watu wasiokubali kustaafu wala kuamini kuwa kila zama kitabu chake pamoja na watu wake. CCM ni chama chenye misingi imara sana na pia kinaongozwa kwa Katiba na Kanuni zake,” alisema Bw Juma na kuongeza kuwa haoni sababu ya kuleta vurugu ndani ya chama wakati zipo taratibu za kufuata.

Bw Juma alisema hatua zinazochukuliwa na viongozi wa kitaifa akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan zina Baraka zote za chama na pia ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Aliwakumbusha wana-CCM kuwa vyama vya TANU na ASP kabla ya kuungana mwaka 1977, vilijielekeza katika suala la ukombozi lakini kuundwa kwa CCM kulenga kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ndicho kinachofanyika sasa.

“Rais mstaafu wa Zanzibar Dkt Salmin Amour alipofanya maamuzi ya kujenga mahoteli alipingwa sana baadhi ya watu bila kujua matokeo ya baadaye,lakini leo matunda ya uwekezaji huo yanaonekana na serikali inapata mapato mengi katika tasnia hiyo.

Bw Juma amewataka wana-CCM kuendelea kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na yule wa Jamhuri ya Muungano ili serikali zao ziwezekutekeleza ilani ya uchaguzi kwa kuwaletea watanzania maendeleo stahiki ya kijamii na uchumi.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bw Ramadhani Shaibu Juma alikemea habari za upotoshaji kuwa Rais  ameuza  visiwa kwani siyo za kweli kwani kilichofanyika ni kuhamasisha uwekezaji  kwenye fukwe ilikuchochea ukuaji wa uchumi.

“Sisi Zanzibar hatuna madini zaidi ya uchumi unaotokana mazao ya bahari na kilimo. Kuhamashisha uwekezaji kwenye fukwe utasaidia kuongeza vipato kwa wakazi wa maeneo husika,” alisema.

“CCM lazima turudi kwenye maadili ya chama. Sisi wa-NEC tuna jukumu kubwa la kuimarisha chama sambamba na kulinda maadili kuanzia ngazi ya Tawi hadi Taifa,” alisema na kuzipongeza serikali mbili kwa kazi nzuri inayofanywa kuwaletea wananchi maendeleo.

Naye, Mjumbe wa  Halmashauri Kuu ya Taifa Mkoa wa Kaskazini Pemba , Bw Omar Zubeir Mbwana alisema ubinafsi miongoni mwa watu wachache ambao pia wanakiuka ahadi zao kwa chama ndiyo chanzo malumbano yasiyo na tija.

“Chama lazima kiwafutilie ‘ magenge’ ya wanachama ndani chama na wale wote wanaothibitika kukiuka maadili na misingi ya chama ni vizuri wakachukukuliwa hatua stahiki za kinidhamu ili kukomesha tabia hizo.

Kauli hizo za viongozi ndani ya chama imekuja kufuatia baadhi ya viongozi wastaafu ndani ya chama kuleta migongano na mivutano isiyo ya lazima na kushindwa kuwaunga mkono viongozi waliopo waweze kutekeleza majumu yao.

Mwenyekiti  mstaafu  wa CCM Mkoa  wa Mjini na Magharibi  Unguja, Bw. Boraafya  Sirima  Juma (katikati) akisisitiza jambo   kwenye mkutano na waandishi wa habari  mjinini Unguja jana akiwataka viongozi  wastaafu  ndani ya chama na serikalini kuunga mkono  juhudi  zinazochukuliwa na  Rais Hussein Ali Mwinyi  katika kuleta  mageuzi ya kiuchumi na kijamii. Kushoto  ni   Bw. Ramadhani Shaibu  Juma  Mjumbe  wa Halmashauri  Kuu ya  Taifa  NEC kutoka Chama cha Mapinguzi (CCM), Mkoa wa Kaskazini Pemba na (kulia) ni  Bw. Omar Zuber Mbwana  Mjumbe  wa Halmashauri  kuu  ya Taifa  Nafasi 4 Mkoa wa Kaskazini Pemba.   

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad