Rais Samia na juhudi za kuondoa tatizo la maji nchini - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 7, 2022

Rais Samia na juhudi za kuondoa tatizo la maji nchini

 METHALI moja ya kiswahili inasema ‘Mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe’ ndivyo tunavyoweza kusema kwenye utendaji kazi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anafanya kazi kubwa ya kujenga taifa na kuleta maendeleo ingawa anapigwa mawe na wengi.


Rais Samia Suluhu aliahidi kuendeleza miradi yote iliyoachwa na watangulizi wake jambo ambalo watu wengi walikua na wasiwasi nalo kwa kudhani kwamba hatoweza, lakini kwa ujasiri alisimama na kuahidi kuiendeleza.

''Hata miradi hii ilivyoanzishwa,ilianzishwa awamu ya tano mimi nikiwa makamu wa Rais. Kwa hiyo ni sehemu ya miradi hiyo kuanza kwake na kutekelezwa kwake. Sasa kwa kunitizama sura na kusema kwamba asingeweza kuendesha hii miradi nadhani hekima haikutumika.'' - Rais Samia Suluhu Hassan , wakati wa uzinduzi wa nyumba 644 za Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam.

Juni 6,2022, Rais Samia Suluhu Hassan alishuhudia utiaji saini wa mikataba ya Miradi ya Maji wa Miji 28, Mikataba hiyo imesainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na makampuni ya JW INFRA Ltd, AFCONS Infrastructures Ltd, Larsen & Toubro, Megha Engineering and Infrastructures Ltd, China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na Jandu Plumbers Limited.

Kupitia mikataba hiyo ni dhahiri kwamba Rais Samia anatekeleza ahadi yake ya kuendeleza miradi yote iliyoanzishwa na kuachwa na watangulizi wake.

Mradi huu wa Maji kwenye Miji 28 ulianza tangu Juni 19, mwaka 2015 ambapo serikali iliingia mkataba wa kuandaa andiko la mradi na upembuzi yakinifu.

Awali, mradi huo ulikuwa utekelezwe katika miji 16 bara na mmoja Zanzibar huku mgawanyo wa fedha ulikuwa dola za Marekani milioni 465 bara na dola za Marekani milioni 35 Zanzibar.

Mei 10, mwaka 2018 serikali iliingia mkataba wa kifedha kati ya serikali na benki ya Exim ya India na michakato mbalimbali iliendelea ambapo baadaye katika mapitio ikaonekana mradi huo unaweza kujengwa miji mingi zaidi hadi kufikia 28.

Msemo wa kwamba mama anaupiga mwingi unaweza kuudhihirisha tena sasa baada ya Rais Samia kuuendeleza mradi huu mkubwa zaidi Tanzania wenye thamani ya Sh1.2 trilioni.

Kati ya fedha hizo zilizotolewa na india, Tanzania bara imepata Dola za Marekani milioni 465 (Sh1.1 trilioni) na kiasi kilichobaki kitapelekwa Zanzibar.

Miji iliyobahatika kupata neema hiyo ni Muheza, Handeni na Pangani mkoani Tanga, Makonde, Nanyumbu na Kilwa Masoko (Mtwara), Ifakara (Morogoro), Chunya na Rujewa (Mbeya) na Songea mkoani Ruvuma.

Miji mingine ni Njombe, Wanging’ombe na Makambako mkoani Njombe, Mafinga (Iringa), Mpanda (Katavi), Sikonge, Urambo na Kaliua (Tabora), Singida, Kihomboi na Manyoni (Singida), Chemba na Chamwino (Dodoma), Kasulu (Kigoma), Kayanga (Kagera) ,Geita na Chato (Geita), Rorya, Mugumu na Tarime (Mara).

Kwa maana hiyo, kuna dalili zote utekelezaji wa Ilani ya CCM ya kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2025 huduma ya majisafi na salama inafikia asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini kwani mpaka sasa upatikanaji wa maji umeshafika 74% kwa vijijini na 86.9% mijini.

Ikiwa mradi huo utatekelezwa kikamilifu utakuwa ndiyo mradi mkubwa zaidi Tanzania kuzidi miradi ya miradi ya Tabora- Igunga-Nzega uliojengwa kwa Sh617 bilioni na mradi wa Arusha wenye thamani ya Sh520 bilioni.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad