HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 10, 2022

RAIS SAMIA ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Queen Sendiga kutokana na vifo vya watu 19 katika ajali ya barabarani.

Ajali hiyo imetokea alfajiri ya tarehe 10 Juni, 2022 katika Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa na kusababisha vifo vya wanaume 14, wanawake 4 na mtoto mmoja wa kike.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi, basi dogo la abiria aina ya Coaster lililokuwa likisafiri kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Iringa liligonga lori lililokuwa limeharibika katika eneo hilo.

Wakati majeruhi wakiwa wanaokolewa lilitokea lori lingine lililopoteza muelekeo na kugonga tena Coaster hiyo pamoja na majeruhi waliokuwa wanaokolewa.

ACP Bukumbi amesema Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Aidha, Rais Samia amevitaka vyombo vyote vinavyosimamia usalama barabarani kuendelea kutoa elimu kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani.

Rais Samia pia anawapa pole wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi. Amina.
ZuhuraYunus

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad