HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 28, 2022

Diaspora Watanzania waipongeza Benki ya CRDB na CPS kwa kuwashirikisha fursa

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mh. Mahmoud Thabit Kombo (wa pili kushoto) akiwa na wawakilishi wa Benki ya CRDB, Mercy Nkini, Meneja Uhusiano kitengo cha Diaspora (kushoto), Emmanuel Kiondo, Meneja Mwandamizi Mawasiliano na Uhusiano (kulia) pamoja na Janerose Mwombela, Meneja wa Mikopo ya Nyumba. Wawakilishi hao wa Benki ya CRDB wapo katika ziara ya nchi za Ulaya ili kuhamasisha Watanzania waishio huku kuwekeza nyumbani.
Ufaransa, Juni 28, 2022 – Kwa takribani wiki mbili maafisa wa Benki ya CRDB kupitia kitengo chake cha Diaspora wamefanya ziara katika nchi za Ulaya ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha Watanzania waishio ughaibuni kuwekeza nyumbani. Ziara hiyo inayofanyika kwa ushirikiano na kampuni ya CPS na TDH (Tanzania Diaspora Hub) imehusisha nchi za Ubeligiji, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Uholanzi, Italia na Sweden ambapo pamoja na mambo mengine imejikita katika kuhamasisha Watanzania wanaoishi nje kuweza kuwekeza na kumiliki nyumba katika miradi mbalimbali nchini.

Meneja Uhusiano wa Kitengo cha Diaspora wa Benki ya CRDB, Bi. Mercy Nkini amesema kuwa Benki ya CRDB imekua na utaratibu kwa kutembelea na kushiriki majukwaa mbalimbali ya diaspora ikiwa ni Benki ya kwanza nchini kuanzisha huduma za diaspora mnamo mwaka 2014 ambazo zilitanguliwa na akaunti maalum kwa diaspora iliyopewa jina la Tanzanite. Hadi sasa zaidi ya Watanzania 30,000 waishio nchi mbalimbali wameweza kufikiwa na kufunguliwa akaunti ya Tanzanite ya Benki ya CRDB.

“Tuna fahamu kuwa Watanzania wengi ambao wanaishi ughaibuni bado wana ndugu na jamaa nyumbani Tanzania, hivyo pamoja na kuwapa akaunti ya Tanzanite ambayo inawawezesha kuweka akiba na kufanya miamala ya kibenki wakiwa ughaibuni, tuliona ni vyema pia kuwashirikisha juu ya fursa za uwekezaji nyumbani pamoja na kuwawezesha kufanya uwekezaji huo kupitia mikopo yetu” alisema Bi. Mercy.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya dunia mwaka 2019, fedha zilizotumwa barani Afrika kwa njia rasmi za kifedha zilifikia takribani Dola za Kimarekani Bilioni 86 ambapo katika hizo asilimia 70 zilipokelewa nchini Misri, Nigeria na Morocco. Kwa upande wa Nigeria, pesa zilizotumwa mwaka 2018(Dola Bilioni 22 za Kimarekani) zilikua ni nyingi kuliko fedha zote za bajeti ya nchi hiyo (Dola Bilioni 18). 

Hii inaonyesha ni kwa kiasi gani fedha zinazotumwa na raia wa nchi wanaoishi ughaibuni zinaweza kutumika katika uwekezaji mkubwa ambao unaweza kuleta tija kwao, familia zao na nchi zao kwa ujumla. 

Kwa upande wake Pamela Assey ambae ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania waishio nchini Ufaransa amesema kuwa wanafurahi kuona Benki ya CRDB inatambua mchango mkubwa wa diaspora katika kujenga uchumi wa nchi  na kuwa pamoja na mambo mengine Jumuiya yao inalenga kuitangaza nchi ambapo wamekua wakiandaa shughuli mbalimbali ikiwemo “Usiku wa Mtanzania” ambao unalenga kutangaza utamaduni na vivutio vya Tanzania.  

 “Pamoja na kutukutanisha na kujenga umoja kati yetu lakini pia tunalenga kuitangaza nchi yetu na kusaidia kiuchumi na kijamii pale inapowezekana hivyo tunafurahi kuona Benki ya CRDB kuweza kushiriki nasi katika “Usiku wa Mtanzania” ambapo wametushirikisha katika fursa nyingi zilizopo nyumbani ikiwemo hii ya kumiliki nyumba ambayo wamekua wakiitangaza kwa kipindi hiki kwa kushirikiana na CPS” aliongeza Pamela.

Akizungumzia mikopo ya nyumba ya Benki ya CRDB, Meneja wa Benki ya CRDB anaehusika na mikopo ya nyumba, Janerose Mwombela amesema kuwa Benki ya CRDB imejipanga vyema kuwawezesha Watanzania wanaoishi ughaibuni kumiliki nyumba ambapo Benki ya CRDB inatoa mkopo wa nyumba wa hadi Bilioni 1 kwa kipindi cha hadi miaka 20 kwa riba nafuu zaidi sokoni. Sambamba na hilo Benki ya CRDB inatoa mkopo wa nyumba kwa Shilingi ya Tanzania na Dola za Kimarekani ili kuweza kukidhi mahitaji ya wateja kutoka ndani na nje ya nchi.  

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad