Benki ya NMB imetoa vifaa
mbalimbali vya afya na vya shule vyenye thamani ya Sh.milioni 27 kwa
Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Shule ya Msingi Kwembe na Shule ya
Sekondari Urafiki ikiwa ni muendelezo wa benki kuchangia katika
maendeleo ya jamii zinazoizunguka.
Akizungumza katika hafla ya
kukabidhi vifaa hivyo, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam,
Donatus Richard alisema wamekabidhi jumla ya vitanda 10 vya kulalia
wagonjwa, vitanda vitano vya kujifungulia, mashine 15 za kupimia presha
na mapazia 10 ya kutenganisha wodi. Kwa upande wa Shule ya Msingi Kwembe
walipata viti na meza 35 za walimu huku Shule ya Urafiki wakipata meza
na viti 110 kwaajili ya wanafunzi.
Meneja huyo aliongeza kuwa
mbali na mengi yanayofanywa na serikali kwaajili ya wananchi, wao kama
wadau wa maendeleo wanao wajibu wa kuendelea kuchangia katika jamii
kwani jamii ndio chanzo cha mafanikio mengi ambayo benki hiyo imekuwa
ikiyapata.
Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, mgeni rasmi
wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kheri James alisema kuwa Benki
ya NMB inastahili pongezi kwani wamekuwa karibu sana sio tu kwa Wilaya
ya Ubungo bali kwa wilaya mbalimbali nchini na wamekuwa wakisaidia sana
hususani katika Sekta ya Elimu na Afya.
“Nitoe wito wangu kwa
watumishi wa hospitali hii na walimu wa shule zinazopokea vifaa hivi,
vifaa hivi vikawe chachu ya maendeleo ya sekta hizi. Tuvitumie vyema kwa
maslahi mapana ya wananchi tunaowahudumia ili kila akifika kupata
huduma akute vifaa hivi vikiwa katika hali nzuri na vitunufaishe,”
aliongeza Mhe Kheri.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya
Ubungo,Jaffari Nyaigesha aliishukuru Benki ya NMB huku akiwaasa
wananchi kuwa chachu ya kuhakikisha misaada hiyo inatumika vyema na
inatunzwa katika hali nzuri ili iwanufaishe wengi zaidi.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo, Dk. Imani Mwanang’ombe
alisema kuwa kwa misaada hiyo hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa
kuhudumia wagonjwa zaidi ya 250 kwa wiki hivyo kupelekea kuwa na uwezo
wa kuhudumia wananchi zaidi ya 1,000 kwa mwezi huku idadi hiyo
ikitazamiwa kuongezeka baada ya kukamilika majengo mengine ya hospitali
hiyo Agosti mwaka huu.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard (wapili kushoto) akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Ubungo, Mhe. Kheri James (wapili kulia)moja ya mashine ya presha katika Hospitali ya wilaya ya Ubungo. Kushoto ni Meneja wa NMB tawi la Ubungo Plaza, Sylvester Ngowi na kulia ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispa ya Ubungo, Mhe. Jaffar Juma Nyaigesha.
No comments:
Post a Comment