WILAYA YA TUNDURU YAIBUA ZAIDI YA WAGONJWA 1,728 WA TB KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MIWILI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 20, 2022

WILAYA YA TUNDURU YAIBUA ZAIDI YA WAGONJWA 1,728 WA TB KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MIWILI

 

Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa Wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole akitoa elimu ya kifua kikuu kwa wakazi wa kijiji cha Matemanga wilayani humo,kampeni hizo zimesaidia sana kuibua watu wengi wenye ugonjwa huo.

Na Muhidin Amri, Tunduru
HOSPITALI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma imefanikiwa kuibua wagonjwa 1,728 wenye maambukizi ya kifua kikuu kuanzia mwaka 2020 hadi Januari 2022.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Wilfred Rwechungura, wakati akielezea mafanikio na mikakati ya kampeni ya kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu inayoendelea katika wilaya hiyo.

Dkt Rwechungura alisema,kuanzia mwaka 2020 Hospitali ya wilaya chini ya kitengo hicho imekuwa na mafanikio makubwa katika
mapambano dhidi ya ugonjwa wa TB kwani kila mwaka imekuwa inavuka malengo wanayopewa na Wizara ya Afya.

Alisema,mwaka 2020 waliwapewa malengo ya kuibua wagonjwa 647, lakini kutokana na mikakati waliyojiwekea na kutekeleza waliibua wagonjwa 709 wanaume 387 na wanawake 322.


Aidha alisema kati ya watu hao walioibuliwa,watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na tano ni 221,na watoto 105 walio chini ya miaka mitano walipata dawa kinga(IPT) na 171 wanaoishi kwenye familia za wagonjwa wa TB ya mapafu walichunguzwa.


Dkt Rwengura aliongeza kuwa,katika kipindi hicho watu waliopimwa virusi vya ukimwi walikuwa 709 ambapo 79 waligundulika kuwa na virusi vya ugonjwa huo na wote wameanzishiwa Dawa.

Kwa mujibu wa Dkt Rwechungura, mwaka 2021 malengo ilikuwa kuibua wagonjwa 741,hata hivyo walifanikiwa kuibua 768 kati yao wanaume 403 na wanawake 365 ambapo watoto walio chini ya miaka 15 walikuwa 289 huku waliopimwa VVU ni 768 na waliokutwa na maambukizi ni 55.

Alisema, mwaka huo 2021 familia za watoto walio chini ya miaka mitano wenye TB ya mapafu ambao walichunguzwa ni 221 na walioanzishiwa dawa kinga walikuwa 179 na watu 13 walipoteza maisha.

Pia alieleza,kwa mwaka 2022 wamepewa malengo ya kuibua wagonjwa 841,lakini katika robo ya tatu iliyoanzia Mwezi Januari hadi Machi,tayari wamefanikiwa kuibua jumla ya watu 251 kati yao wanaume 139 na wanawake 112.

Kwa mujibu wake,katika muda huo watoto walio chini ya umri wa miaka 15 waliogundulika kuwa na TB ni 77 na waliopima VVU walikuwa 251 ambapo watu 9 wamekutwa na maambukizi na wote wameanzishiwa Dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo .

Naye Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole alisema,katika malengo ya mwaka huu Hospitali ya wilaya imepewa lengo la kuibua wagonjwa 200,Hospitali ya Misheni Mbesa 150,Hospitali ya Kiuma 100,vituo vinavyopima makohozi Matemanga wagonjwa 15,Nakapanya 15,Mkasale 15,Mtina 15,Mchoteka 15 Zahanati ya Nandembo 10 na Namiungo wagonjwa 10.

Mkasange alieleza kuwa,katika miaka mitatu tangu kuanza kwa kampeni kabambe ya uelimishaji na uibuaji wa ugonjwa huo kumekuwa na mafanikio makubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Alisema,mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mkubwa wa watumishi wa idara ya afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi wa Hospitali ya wilaya na wahudumu ngazi ya jamii.

Alisema, wahudumu ngazi ya jamii wamekuwa msaada mkubwa katika kampeni hizo kwa kuwa wanaokwenda kwenye mikusanyiko ya watu ikiwamo shule za bweni na maeneo mengine kwa ajili ya kutoa elimu ya kifua kikuu na kuchukua sampuli za makohozi na kupeleka Hospitali kwa ajili ya vipimo.

Aidha,amewashukuru wadau Shirika la MDH-Amref Heath Africa kwa mchango mkubwa wanaotoa wa kuwapa mafunzo wahudumu ngazi ya jamii na watumishi wa afya ambayo yamesaidia sana kuongeza morali ya utendaji na uwajibikaji.

Mkasange amevipongeza baadhi ya vyombo vya Habari ikiwamo Gazeti la Habarileo na Itv kwa mchango mkubwa, kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu.

Kwa mujibu wa Dkt Mkasange,ugonjwa wa TB unatibika kwa mtu aliyeambukizwa na mwenye dalili za ugonjwa huo kufika Hospitali kwa ajili ya uchunguzi na anayeabainika anaanzishiwa matibabu na kuacha mila potofu zinazohusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina.

Mkazi wa Tunduru aliyewahi kuugua ugonjwa wa kifua kikuu na kupoma Salome Golihama,ameishukuru serikali kuhamasisha jamii kujitokeza kwenye kampeni na elimu ya kifua kikuu kwa wananchi.

Alisema,hatua hiyo imesaidia sana jamii kufahamu dalili za ugonjwa huo na kujitokeza kwa hiari kupima na kuanza matumizi ya dawa ambazo zinatolewa bure.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad