HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 11, 2022

MSIGWA-SERIKALI IPO KWENYE MAZUNGUMZO NA WAWEKEZAJI JUU YA UJENZI WA BANDARI YA BAGAMOYO



 

Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo,Gerson Msigwa akizungumza wakati wa ziara ya Maafisa Habari wa Wizara na Taasisi za Umma nchini katika Bandari ya Tanga ambao wapo Jijini Tanga wakiendelea na kikao chao
Sehemu ya Maafisa Habari wa Wizara na Taasisi za Umma wakiwa kwenye Bandari ya Tanga wakati wa ziara hiyo

NA OSCAR ASSENGA,TANGA.

SERIKALI ipo na mazungumzo na wawekezaji juu ya mpango wa ujenzi wa Bandari mpya ya Bagamoyo mkoani Pwani ili kusogeza huduma karibu na wananchi na hivyo kuchangia kukuza pato la Taifa na wananchi kwa ujumla.


Hayo yalisemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo,Gerson Msigwa wakati wa ziara ya Maafisa Habari wa Wizara na Taasisi za Umma nchini katika Bandari ya Tanga ambao wapo Jijini Tanga wakiendelea na kikao chao

Alisema kwa sasa wamerejesha mazungumzo hayo baada ya Rais Samia Suluhu kupitia serikali yake ya awamu ya sita kuona ni vyema wakarejesha mazungumzo hayo na kukubaliana maeneo serikali itayoona ina maslahi nayo pamoja na wawekezaji ili wautekeleze mradi huo.


Alisema huo mradi huo ni mkubwa na wakifanikiwa kuutekeleza utasaidia kuchochea kasi ya maendeleo na hivyo kuchangia pato la wananchi na Taifa kwa ujumla ikiwemo kufungua milango ya uwekezaji hapa nchini.


Alisema sio Bandari bali patajengwa Viwanda, kwasababu eneo hilo wanakusudia kulifanya liwe kanda maalumu ya kiuchumi ya Bagamoyo pale panajengwa bandari, Viwanda, eneo la makazi ,maduka makubwa na sehemu nyingi za kibiashara ikiwemo ujenzi wa viwanda takribani 1000 na hivyo itawezesha kuwa kanda maalumu ya viwanda.


Akizungumzia ujenzi wa Bandari unaoendelea katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara Msigwa alisema wamewapeleka maafisa habari wa serikali ili waone kazi kubwa inayotekelezwa na serikali ili wananchi wanapotaka kujua nini serikali inafanya katika fursa ya uchumi wa bluu ili wajue kwamba kuna kazi kubwa inayofanyika.


"Niwaambie kwamba hii moja kati ya kazi kubwa ambazo zinafanyika hapa Tanga lakini pia tunafanya kazi kama hizi kwenye maziwa yetu ikiwemo Kigoma, Kalema kule kwenye ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria pia pale Mwanza tumejenga cholezo kubwa na ujenzi wa meli unaendelea kule kwa hiyo kuna kazi nyingi serikali inafanya,kwenye maeneo haya na tungependa maafisa habari wetu wajionee wao wenyewe na kupeleka huu ujumbe mzuri kwa wananchi, "Alibainisha Msigwa.


Akizungumzia miundombinu ya reli Msigwa alisema serikali imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha treni zinarejea Mkoani Tanga mpaka Arusha ambapo hivi sasa kazi inayokwenda kufanyika ni ya kuimarisha miundombinu hiyo na kuona namna bora ya kuja na reli nzuri zaidi.


Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo,Mhandisi wa bandari ya Tanga Hamis Omari Kipalo amesema kwa upande wa ujenzi wa gati namba moja na namba mbili katika bandari hiyo umefikia asilimia 45 mpaka sasa.


Mhandisi huyo alisema mradi wao kimkataba unatakiwa kukamilika tarehe 16 mwezi octoba mwaka huu.


Baadhi ya maafisa habari waliotembelea bandarini hapo wamesema ziara hiyo imewasaidia kuona namna serikali ilivyojizatiti kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.


David Mwaipaja ni Afisa mahusiano na mauzo kutoka Watumishi Housing Investment amesema kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika bandari zetu ambazo zipo kwenye miradi ya kimkakati jambo ambalo litakuwa chachu kwa maafisa habari kuchukua na kwenda kuisemea serikali kwa wananchi ili mambo yasiyoonekana kiurahisi kwa wananchi basi yaweze kuwafikia sawasawa na serikali inavyofanya.


Upanuzi wa ujenzi wa mradi wa gati za kisasa katika bandari nchini unatarajiwa kufungua fursa za kibiashara ambapo ujenzi huo umefanyika katika Mikoa ya Tanga, Mtwara na Daresalaam.


Kwa upande wa bandari ya Daresalaam jumla ya shilingi trilioni moja nukta mbili zinatarajiwa kutumika kwajili ya ujenzi wa gati sambamba na kununua vifaa vitakavyorahisisha utoaji wa huduma ikiwemo upakuaji wa shehena.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad