Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango
amesema eneo huru la kibiashara barani Afrika ni fursa kubwa kwa nchi za
bara hilo katika kukuza uchumi na maendeleo.
Makamu
wa Rais amesema hayo wakati wa majadiliano maalum ya viongozi wakuu wa
nchi za Afrika yalioshirikisha wadau na marafiki wa nchi za Afrika
kutoka mataifa mengine, majadiliano yaliofanyika katika mkutano wa
Jukwaa la Uchumi Duniani unaoendelea Davos nchini Uswisi.
Amesema
katika kutumia fursa hizo nchi za Afrika zinapaswa kupunguza vikwazo
mbalimbali ikiwemo vya kikodi katika ufanyaji biashara pamoja na
kuimarisha miundombinu itakayorahisisha biashara hizo katika eneo hilo
huru.
Ameongeza
kwamba ni muhimu kuwekeza katika teknolojia itakayorahisisha kufanya
biashara na malipo mbalimbali pamoja na kufanya ubia na sekta binafsi,
mashirika ya kimataifa na mataifa mengine ili kuongeza uzalishaji katika
viwanda.
Makamu
wa Rais amesema Tanzania inaendelea kuhakikisha wananchi wanaelewa
fursa zilizopo katika eneo huru la biashara barani Afrika pamoja na
kuimarisha sekta ya uwekezaji kwa kuingia ubia na wadau mbalimbali ndani
na nje ya bara la Afrika ili kuweza kufanya biashara katika ukanda huo
huru kwa tija zaidi.
Katika
hatua nyingine Makamu wa Rais ameshiriki katika mjadala uliohusu
ufufuaji uchumi pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kurejesha
amani na mtangamano duniani ambapo viongozi hao wamejadili namna ya
kushirikiana katika kukabiliana kutatua matatizo ya kisiasa
yanayopelekea vita na migogoro.
Aidha
Makamu wa Rais amesema ni muhimu dunia inapokabiliana na changamoto
kama vita kutosahau changamoto zingine ikiwemo upungufu wa chakula
pamoja na kuhakikisha Afrika inashirikishwa katika maamuzi mbalimbali ya
dunia. Amesema Afrika ina fursa kubwa ya kuchangia katika kuleta amani
na suluhisho la upatikanaji wa chakula kama itaungana na mataifa mengine
kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Makamu
wa Rais Makamu wa Rais yupo Davos nchini Uswisi kumwakilisha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika
mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani unaoshirikisha wakuu wa nchi, wakuu
wa taasisi na mashirika ya kimataifa pamoja pamoja na wafanyabiashara.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango
akizungumza wakati wa majadiliano maalum ya Viongozi Wakuu wa Nchi za
Afrika yalioshirikisha wadau na marafiki wa Nchi za Afrika kutoka
mataifa mengine, majadiliano yaliofanyika katika mkutano wa Jukwaa la
Uchumi Duniani unaoendelea Davos nchini Uswisi. Mei 24, 2022.
No comments:
Post a Comment