HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 21, 2022

Maelfu ya wanafunzi kufaidika na miradi ya madarasa, vyoo Karagwe

Wanafunzi wakiwa kwenye moja ya Darasa lililopitiwa na miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.


Matukio mbalimbali wakati wa Uzinduzi wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Na Mwandishi wetu, Kagera
JUMLA ya wanafunzi 3,100 wameanza kufaidika na miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera iliyotekelezwa na shirika la Jambo for Development kwa ushirikiano na serikali na jamii.

Miradi hiyo iliyozinduliwa jana imetekelezwa katika shule za msingi za Kijumbura yenye wanafunzi 1,400 ambako madarasa manne yamejengwa na shule ya Nyakahanga yenye wanafunzi 1,700 ambako matundu 20 ya vyoo yamejengwa ikiwa ni pamoja na chumba maalum cha wasichana kujisitiri wakiwa katika hedhi pamoja na choo maalumu kwa ajili ya walemavu.

Thamani ya miradi yote miwili ni Tshs 132, Jambo for Development ikifadhili asilimia 60 ya gharama--Tshs 79.2 Milioni huku halmashauri ya wilaya ilichangia asilimia 30 na wananchi asilimia 10 ya thamni ya miradi hiyo.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa wilaya ya Karagwe katika shule ya Nyakahanga, Afisa Elimu wa wilaya, Bw. Aloyce Maira amesema kazi iliyofanywa na shirika hilo ni ya kizalendo na kupongezwa. Aliliomba shirika hilo pamoja na wadau wengine ndani na nje ya mkoa wa Kagera kuendelea kusaidia shule hiyo kongwe iliyojengwa mwaka 1924 na nyingine katika halmashauri hiyo.

“Sisi kama halmashauri tuko tayari kuchangia asilimia 30 pale ambapo wadau wa maendeleo watakuwa tayari kuja kutusaidia,” alisema Bw. Aloyce.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyakahanga, Jonitha Clavery alitoa shukrani kwa ofisi ya Mkurugenzi wa wilaya, shirika la Jambo for Development na wananchi kwa kujitoa kwao kwa faida ya wanafunzi na maendeleo ya wilaya hiyo.

Afisa Mawasiliano wa shirika hilo, Bw. Lameck Kiula alisema ongezeko la madarasa manne katika shule ya Kijumbura litasaidia kupunguza uwiano wa watoto katika darasa moja kutoka 180 hadi 111 na hivyo kuendelea kuboresha mazingira ya shule kwa watoto na waalimu.

“Lengo ni kutomuacha mtoto yeyote nyuma kwa sababu ya jinsia yake au ulemavu,” alisema Bw. Kiula.

Mwanafunzi Anitha Peter katika shule ya msingi ya Nyakahanga darasa ya Saba alisema uwepo wa chumba maalumu cha wasichana kujihifadhi wakati wa hedhi umekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wa kike shuleni hapo.

“Tunashukuru sana. Huu ni ukombozi kwetu. Mwanzo tuliteseka sana na hata kutohudhuria shuleni,” alisema.

Jambo for Development imejikita katika kuboresha elimu, afya na usawa wa kijinsia mkoani Kagera kwa kutumia mbinu ya michezo ili kuwaunganisha wadau mbalimbali kutekeleza malengo hayo. Mbali na Karagwe, miradi mingine iko katika halmashauri za wilaya za Kyerwa, Ngara, Biharamuro, Muleba, Bukoba DC, Misenyi na Bukoba Manispaa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad