HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 20, 2022

Dkt Tulia avutiwa na utendaji wa Benki ya CRDB katika kutengeneza faida

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kutengeneza faida kubwa inayoiwezesha benki hiyo kutoa gawio kwa wanahisa wake kutokana na uwekezaji wao ndani ya benki hiyo. 

Dkt. Tulia alitoa pongezi hizo wakati akifungua semina ya elimu ya fedha iliyoandaliwa na benki hiyo kwa wanahisa wake na Watanzania kuelekea Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa utakaofanyika Mei 22, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

“Nadhani sitakuwa nimekosea nikisema ongezeko la faida baada ya kodi ambayo Benki yetu ya CRDB imepata mwaka jana kufikia Sh bilioni 236 kulinganisha na Sh bilioni 165 mwaka 2020, ni ukuaji mkubwa wa faida kupata kutokea,” alisema Dkt. Tulia.
Alisema kuwa Benki ya CRDB imeendelea kudhihirisha kivitendo kuwa “Benki kiongozi” nchini kwani kila mwaka imekuwa ikiendelea kutoa faida ya uwekezaji kwa wanahisa wake huku akizitaka taasisi nyengine za umma na binafsi kuiga mfano.

“Nimefurahishwa pia kusikia mwaka huu Bodi ya Wakurugenzi imekuja na pendekezo la ongezeko la asilimia 64 ya gawio kwa hisa. Wanahisa wa Benki ya CRDB mnastahili kutembea kifua mbele kwa ongezeko hili,” aliongezea Dkt. Tulia.
Dkt. Tulia pia aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina ya elimu ya fedha na uwekezaji kwa ajili ya wanahisa wake na Watanzania huku akibainisha kuwa umahiri wa masuala ya fedha wa wananchi ni moja ya msingi muhimu wa maendeleo ya watu wa taifa lolote duniani.

“Niwapongeze Benki ya CRDB kwa kuongoza katika utoaji wa elimu ya masuala ya fedha kwa Watanzania. Siku chache zilizopita, mliandaa semina mliyoiita CRDB Bank Uwekezaji Day, mimi niliichungulia mtandaoni nikiwa Dodoma.,” Dkt. Tulia alisema huku akiitaka benki hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza ujumuishi wa kifedha.
Aidha, Dkt. Tulia aliiitaka Benki hiyo kuendelea kuwekeza katika kuendelea kuwezesha sekta mbambali za maendeleo nchini hususan sekta ya kilimo, huku akiitaka pia kusaidia malengo ya Serikali katika uanzishwaji wa Benki ya Ushirika ya Taifa kama ambavyo imefanya kwa Benki ya Ushirika ya Tandahimba (TACOBA) na Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL). Dkt. Tulia pia aliitaka Benki kuendelea na jitihada za uwezeshaji wa kundi la vijana ili kuchochea ukuaji wa ajira nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alisema benki hiyo ikiwa benki ya kizalendo inayomilikiwa na Watanzania kwa zaidi ya asilimia 80, inajivunia kuendelea kukuza thamani ya uwekezaji wa wanahisa wake ikiwamo Serikali ambayo inamiliki asilimia 36 ya hisa katika benki hiyo.

 “Niwakaribishe Watanzania wengine waje kuwekeza ndani ya Benki yetu ili nawao waanze kunufaika na gawio nono ambalo limekuwa likitolewa na Benki yao,” aliongezea Dkt. Laay.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela alisema malengo ya semina hiyo ni kuwajengea uwezo Wanahisa wao pamoja na Watanzania wengine ili kuwajengea uwajibikaji wa kifedha na kuongeza ushiriki katika fursa za uwekezaji hususan katika soko la hisa la Da es Salaam.

“Kwa kutoa elimu hii Wanahisa wetu pia wanapata kufahamu zaidi faida za kuwekeza katika Benki yao ya CRDB, hivyo basi kuongeza uwekezaji na kupata faida nono zaidi, lakini pia kuwahamasisha na Watanzania wengine pia kuwekeza katika hisa hususan za Benki ya CRDB na kuanza kupata gawio,” aliongezea Nsekela.
Nsekela alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha Wanahisa katika Mkutano Mkuu utakaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC) na kupitia Mtandao. “Mkutano utaanza saa 3 asubuhi, watu wa mtandaoni wataweza kujiunga kupitia link https://escrowagm.com/crdb/login.aspx au kupitia SimBanking App,” alisema Nsekela.

Benki ya CRDB imeweka muongozo wa jinsi ya kushiriki mkutano mkuu kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yake ya www.crdbbank.co.tz, mitandao yetu ya kijamii ya Instagram, twitter, lakini pia maelekezo yametumwa kwa ujumbe mfupi kwa Wanahisa.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Tulia Ackson akiwasili katika Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB iliyofanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimitaifa cha Arusha (AICC), kuelekea Mkutano Mkuu wa 27 Wanahisa wa Benki ya CRDB utakayofanyika kesho tarehe 21 Mei 2022. Walioongozana naye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, pamoja na Mwenyekiti wa Bodi Benki ya CRDB, Dkt Ally Laay (kulia).
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Frank Mwaisumbe akizungumza kwenye Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB iliyofanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimitaifa cha Arusha (AICC), kuelekea Mkutano Mkuu wa 27 Wanahisa wa Benki ya CRDB utakayofanyika kesho tarehe 21 Mei 2022.
Mbunge wa Jimbo la Arusha, Mrisho Gambo akizungumza kwenye Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB iliyofanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Kimitaifa cha Arusha (AICC), kuelekea Mkutano Mkuu wa 27 Wanahisa wa Benki ya CRDB utakayofanyika kesho tarehe 21 Mei 2022.







 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad