HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, April 29, 2022

WAJASIRIMALI WATAKIWA KUREJESHA MIKOPO YA SH.MILIONI 267 MAGU

 NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza

SERIKALI wilayani Magu imevitaka vikundi vya ujasiriamali vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kuwa waaminifu na waadilifu kurejesha mikopo hiyo iwanufaishe na wengine.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo,Salum Kalli,kuhusiana na baadhi ya vikundi wilayani humo kusuasusa kurejesha fedha walizokopeshwa ziwawezeshe kujikwamua kiuchumi.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Magu,mwaka 2018 hadi 2021 ilitoa mikopo ya sh. milioni 515.7 kwa vikundi zaidi ya 119 kutoka kwenye mapato ya ndani na kati ya fedha hizo sh.248,166,804 zimerejeshwa na kuwataka wanufaika wa fedha hizo kuwa waaminifu na waadilifu.

“Tulitoa mikopo bila riba ya sh. 515,712,250 na zote zilikwenda kwa walengwa,baadhi vimerejesha kwa wakati lakini bado sh.267,545,451 zimeendelea kubaki mikononi mwa vikundi vilivyonufaika,tutasimamia sheria kuwezesha fedha hizo zirejeshwe,”alisema Kalli.

Alisema changamoto hiyo inasababishwa na baadhi ya wanavikundi kupewa fedha na kuzigawana kila mmoja anafanyia kazi nyingine tofauti na waliyoombea mkopo,wakishindwa wanaanza kurukaruka.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha hizo ni kuwanusuru wananchi na umasikini na wajikwamue kiuchumi.

Alisistiza serikali haitawafumbia macho wajasiriamali wanaotaka kukwamisha mipango yake vikiwemo vikundi vitakavyoshindwa kurejesha fedha walizokopa na Magu haitakuwa kichaka cha vikundi hewa.

“Hatuna vikundi hewa bali havijarejesha mikopo yao kwa wakati,wamepitiliza muda na hivyo tutaanza msako wa kuwatafuta nyumba kwa nyumba warejeshe fedha hizo kabla ya Mei 30,mwaka huu, tunataka wazirejeshe tuzipangie matumizi ziwanufaishe na wengine,”alisema Kalli.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mpandalume Simon,alisema wajasiriamali waliokopeshwa kushindwa kurejesha mikopo wanaikwamisha halmashauri hiyo kuwahudumia wengine pia wanajikwamisha wenyewe kupata mikopo mingine.

“Serikali kutoa mikopo isiyo na riba kwa wananchi wajasiriamali ilikuwa na nia njema,hatutaki kukimbizana nao hasa vijana, waje wenyewe warejeshe fedha zinufaishe n wengine,”alisema Simon.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli (katikati) jana akizungumza na waandishi wa habari (haapo pichani) kuhusu wajasiriamali kurejesha mikopo ya halmashauri kwa kusuasua.Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo (DED Federica Myovella na kulia i Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mpandalume Simon.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu,Mpandalume Simon, akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) jana kutokana na mkwamo wa wajasriamli waliokopeshwa mikopo na halmashauri kushindwa kurejesha.Picha zote na Baltazar Mashaka

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad