HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 30, 2022

Benki ya CRDB yakutanisha wadau wa mpira wa kikapu nchi nzima

Benki ya CRDB imefanya mkutano na viongozi wa mpira wa kikapu kutoka Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) na vyama vya mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani kujadili maendeleo ya mchezo wa mpira wa kikapu nchini hususan mashidano ya CRDB Bank Taifa Cup ambayo imekua ikiyadhamini kwa miaka miwili mfululizo. 

Mkutano huo umefanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB na ukishuhudiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lililowakilishwa na Afisa Michezo Mkuu, Allen Alex.Akizungumza kwa niaba ya Benki ya CRDB, Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano na Uhusiano, Emmanuel Kiondo alisema kuwa Benki ya CRDB ina dhamira ya dhati ya kukuza mchezo wa Kikapu nchini ili kuweza kutoa fursa kwa vijana wengi kuonyesha vipaji vyao na kuvitumia kama sehemu ya kujiingizia kipato. 

“Sote tunatambua kuwa michezo ni ajira na zipo fursa nyingi ambazo zinaweza kupatika kwa vijana kupitia mchezo huu ambao ni miongoni mwa michezo maarufu duniani ambayo Benki ya CRDB imedhamiria kuufanya kuwa sehemu ya ajira kwa vijana lakini pia kutoa fursa za elimu kupitia ufadhili wa masomo kupitia mashindano ya CRDB Bank Taifa Cup” alisema Kiondo.

Kwa upande wake Afisa Michezo Mkuu wa Baraza la Michezo Taifa (BMT), Allen Alex amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza nguvu kubwa katika michezo na hivyo vyama vya michezo na mashirikisho yanapaswa kutumia fursa hii vizuri ili kuweza kupiga hatua kwa haraka. 

“Nitoe wito kwa vyama na vilabu kuhakikisha wanajisajili ili kuweza kutambulika kisheria na kuhakikisha wanahusika kikamilifu katika kutoa mapendekezo ya kuboresha kanuni na sera za michezo ili kukukuza sekta ya michezo nchini” aliongeza Allen. 

Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Rwehabura Barongo alisema tangu kuingia madarakani mwishoni mwa mwaka jana wameweza kuandaa mkakati wa muda mfupi na mrefu wa shirikisho huku wajikita katika kuboresha utawala bora kuanzia ngazi ya shirikisho hadi ngazi ya vyama vya mikoa ili kuboresha usimamizi wa mchezo huo chini. 

Katika mkutano huo viongozi wa mikoa walionyeshwa kufurahishwa na Benki ya CRDB kuendelea kudhamini mashindano ya Taifa Cup huku wakipongeza uamuzi wa kuwakutanisha viongozi ili kushiriki kutoa mawazo yao kama sehemu ya maandalizi ya shindano la CRDB Bank Taifa Cup kwa mwaka 2022. 

Mashindano ya CRDB Bank Taifa yameibua upya hamasa ya mpira wa Kikapu nchini ambapo pamoja na kutoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao, pia mashindano hayo yamekua yakitoa ufadhili wa masomo kwa vijana ambao wamekua wakifanya vizuri katika mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad