WADAU
wa haki za wanawake Pemba wameiomba serikali kufanyia marekebisho
baadhi ya sheria zinazokwaza ufikiaji wa usawa wa kijinsia kwa wanawake
ili kuwezesha ushiriki sawa wa kijinsia katika fursa mbalimbali.
Hayo
yametolewa kwa nyakati tofauti wakati wa mdahalo wa wadau uliolenga
kujadili changamoto za kisheria zinazowakwaza wanawake kushiriki katika
nafasi za uongozi katika Wilaya za Micheweni, Wete, Chake chake na
Mkoani Pemba ulioandaliwa na taasisi ya PEGAO kwa kushirikiana na Chama
cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar) ikiwa ni
kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.
Walisema uwepo
wa sheria hizo Zanzibar unarejesha nyuma juhudi za wanawake kujitokeza
kushiriki katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
Safia Saleh
Sultan, mwanasheria kutoka kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, (ZLSC),
alitaja baadhi ya sheria zinazokwaza ushiriki wa wanawake katika uongozi
kuwa ni; Sheria ya watumishi wa Umma No.3/2003, Sheria ya Mahakama ya
Kadhi No.7/2001, Sheria ya Vyama vya Siasa (1992) na Sheria ya Uchaguzi
no 4/2018, ambapo sheria hizo zimeweka masharti magumu kwa wanawake
wanapohitaji kugomea nafasi za uongozi.
Alisema kutokana na
masharti ya sheria hizo kuwa ngumu kwa wanawake watumishi wa umma
inapelekea kukosekana kwa wanawake wenye uwezo mzuri wa kiutendaji
katika ngazi za maamuzi.
“Wanawake wengi wanaofanya kazi
Serikalini na walio na uwezo mzuri wanaogopa kuingia kugombea nafasi za
siasa na kuitumia haki yao ya msingi ya kikatiba kwa kuhofia kupoteza
nafasi zao kazini kutokana na masharti ya kisheria kuwa magumu,”
alieleza.
Alieleza wakati dunia ikiwa katika maadhimisho ya siku
ya wanawake duniani ni muhimu kuongeza ushawishi wa maboresho ya sheria
hizo ili zitoe fursa kwa makundi yote kushiriki kaika nafasi za uongozi
bila vikwazo.
Alisema, “tukiwa kama ni wadau wakuu wa maswali
haya ya kutetea haki za wanawake na uongozi na wadau wa Sheria, ni vyema
sote kwa pamoja tukashirikiana kuhakikisha kwamba kwamba Sheria hizi
zinafanyiwa utetezi wa maboresho ili ziweze kukidhi misingi ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora nchini.”
Mkuu wa mkoa wa kaskazini
Pemba, Salama Mbarouk Khatib, alisisitiza wanawake kutumia maadhimisho
ya siku ya wanawake duniani kutahimini changamoto zinazowakwaza katika
nyanja mbalimbali na kuzitumia kuwa fursa ya kufikia ukombozi wa
mwanamke.
“Kuelekea siku ya wanawake duniani, sisi wanawake
tunatakiwa kujitathimini kwa zile changamoto ambazo zinatukwaza kufikia
malengo yetu na tuzigeuze kuwa fursa ya kufikia upatikanaji wa haki zetu
na sio kulaumiana,” alisema Salama.
Sabahi Musa Said, mshiriki
wa mdahalo huo alisema ili kufikia ushiriki sawa wa wanawake katika
nafasi za uongozi ni lazima kuwepo kwa sheria zinazolazimisha usawa wa
kijinsia katika kila nafasi.
Alieleza, “kuwepo kwa sheria
lazimishi kuhusu usawa wa kijinsia kwa wanawake kushiriki katika kila
nafasi za uongozi ndiyo itasaidia kufikia lengo la asilimia 50% katika
ngazi zote.”
Kwa upande wake Hasina Ibrahim, mwanachama wa chama
cha Mapinduzi CCM alishauri kufanyiwa marekebisho ya ukomo wa miaka kwa
wabunge na wawakilishi ili kutoa fursa zaidi kwa wengine kushiriki
nafasi hizo.
“Ikiwa rais anawekewa ukomo wa miaka 10 kwanini
mbunge anaongoza maisha.? Wawakilishi na wabunge wakishakaa miaka 10
kama rais wasirudi wapishe wengine kwasababu Wanawake wengi tunashindwa
kupita kwasababu ya rushwa kwa baadhi ya wabunge na wawakilishi kutumia
nguvu na uwezo wao kifedha kushawishi wapiga kura,” alisema Hasina.
Nae
Salma Haji Mcha, spika wa serikali ya wanafunzi katika shule ya
Sekondari Uweleni, Wilaya ya Mkoani Pemba alisema Watoto wa kike
kutokuaminiwa uwezo wao mapema katika nafasi za uongozi bado ni
changamoto kubwa inayopelekea wanawake kushindwa kupewa fursa za
uongozi.
Alieleza, “mwanzoni nilipoingia shule nilitaka nigombee
urais lakini mmoja wa walimu akaniambia kabisa hata kama nikipata kura
zote hawezi kunipitisha nikawa rais kutokana na mimi ni mwanamke.”
Aidha
aliongeza kwamba ili kufikia usawa wa kijinsia jamii inahitajika kuwa
na utayari wa kumuinua mwanamke katika kila fursa na si kumuangusha.
Mapema
mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi Said, alisema PEGAO kwa kushirikiana
na TAMWA Zanzibar wameandaa midahalo hiyo kwa lengo la kujadili Pamoja
changamoto kisheria zinazowakwaza wanawake ikiwa ni utekelezaji mradi wa
ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi unaofadhiliwa na Ubalozi
wa Norway.
“Tukiwa tunaelekea siku ya wanawake duniani,
tumekutana kwa lengo la kujadili changamoto za kisheria zinazowakwaza
wanawake katika harakati za uongozi ili kuhakikisha tunapata kufikia
suluhisho la usawa wakijinsia kwa kila nyanja,” Hafidh Abdi, Mkurugenzi
PEGAO.
Katika mdahao huo uliofanyika kwenye wilaya Nne za Pemba,
jumla ya Sheria tisa zinazokwaza ushiriki wa wanawake katika masuala ya
uongozi zimejadiliwa na wadau hao ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya Siku
ya wanawake duniani yanayofanyika machi nane kila mwaka ambapo kauli
mbiu ya wadau ni ‘Haki na Usawa wa Kijinsia katika Nafasi za Uongozi kwa
Maendeleo Endelevu.’
Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba akizungumza wakati wa mdahalo Mkurugenzi wa PEGAO, Hafidh Abdi Said akizungumza wakati wa mdahalo
mwanasheria kutoka kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, (ZLSC), Safia Saleh Sultan akiwasilisha mada wakati wa mdahalo.
Tuesday, March 8, 2022

Home
HABARI
Wadau Wa Haki Za Wanawake Pemba Washauri Mabadiliko Ya Sheria Zinazokwaza Ushiriki Wa Wanawake Kwenye Uongozi
Wadau Wa Haki Za Wanawake Pemba Washauri Mabadiliko Ya Sheria Zinazokwaza Ushiriki Wa Wanawake Kwenye Uongozi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment