NMB yamkabidhi Rais Samia vifaa vya Elimu kwa Wenye Uhitaji vya Sh Mil. 58/- - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 8, 2022

NMB yamkabidhi Rais Samia vifaa vya Elimu kwa Wenye Uhitaji vya Sh Mil. 58/-

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameishukuru na kuipongeza Benki ya NMB kwa mchango unaoenda kufanikisha uboreshaji elimu kwa makundi maalum, ambako imetoa msaada wenye thamani ya Sh. Mil. 58, wa vifaa mbalimbali, vikiwemo vya kusaidia kuona na kusikia kwa shule 4 jijini Dar es Salaam.

Rais Samia alitoa poongezi hizo wakati wa ziara maalum katika Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Kariakoo, iliyolenga kufanikisha maboresho mbalimbali ya elimu wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma katika shule za sekondari Benjamin Mkapa, Uhuru Mchanganyiko na Jangwani, na Shule ya Msingi Uhuru Wasichana.

Katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu NMB, Ruth Zaipuna, aliyemkabidhi Rais Samia vifaa maalum 60 vya kusaidia wanafunzi wenye uziwi, vifaa 90 vya kusaidia wenye ulemavu wa macho – vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 24, pamoja na kompyuta mpakato ‘laptop’ 20 zenye thamani ya Sh. Mil. 20 na vifaa vya michezo vya Mil. 14.

“Serikali imetumia Sh. Bil. 5.9 katika uboreshaji elimu ngazi ya awali, msingi, sekondari na vyuo, ili kuhakikisha wenye mahitaji wote wanapata elimu nchini. Nawashukuru sana NMB kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu Ruth Zaipuna, kwa kubeba changamoto za vifaa mbalimbali kwa wanafunzi wa shule hizi.

“CEO wa NMB hapa amenikabidhi vifaa vya kusaidia usikivu, uoni na hata kompyuta mpakato 20, ombi langu kwenu ni kutuongezea ‘laptop’ kama hizo kwa sababu shule hizi ni nyingi na mahitaji ya hizo kompyuta ni mengi. Tunawaomba mtusaidie katika hili ili kupunguza changamoto hiyo kwa vijana wetu,” alisisitiza.

Akizungumza wakati akimkabidhi msaada huo, CEO wa NMB, Zaipuna alisema: “Mheshimiwa Rais, NMB ni mdau mkubwa wa elimu Tanzania, ndio maana tumekuja hapa kukuunga mkono katika jitihada za Serikali yako za kuhakikisha Watanzania wanapata elimu bora.

“Tumekuja hapa na vifaa vya kusaidia kuona 90, vya kusaidia kusikia 60, ‘laptop’ 20, pamoja na vifaa vya michezo katika shule hizi.

“Misaada hii inayolenga kusaidia wanafunzi wa shule hizi, tunaamini itaenda kupunguza kwa asilimia kubwa changamoto zilizoelezwa katika risala ya shule ya sekondari ya Benjamini Mkapa, huku vifaa vya michezo tukiamini vitasaidia kuboresha michezo kwa ustawi wa afya za wanafunzi wetu katika shule husika,” alisema Zaipuna.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, aliitaja NMB kama ‘mkono wa kulia wa Serikali ya mkoa’ wake, kwa namna inavyojitoa kupambana na maboresho kwenye Sekta ya Elimu na miundombinu yake, lengo likiwa kuunga mkono jitihada za kufanikisha elimu bora kwa wanafunzi wa mkoa wake.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, (kushoto) akipokea Vifaa vya kusaidia kusikia kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, ikiwa ni msaada wa benki hiyo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, Uhuru Mchanganyiko, Jangwani, na Shule ya Msingi Uhuru Wasichana, wakati wa ziara ya Rais kutembelea shule hiyo katika hafla maalumu ya Uboreshaji Elimu kwa kuzingatia mahitaji maalum. Katika hafla hiyo Benki ya NMB ilikabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Tsh. milioni 58.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, (kushoto) akipokea Vifaa vya michezo na Jezi kutoka kwa Ofisa Mtendaji mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, ikiwa ni msaada wa benki hiyo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wa Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa, wakati wa ziara ya Rais kutembelea shule hiyo katika hafla maalumu ya Uboreshaji Elimu kwa kuzingatia mahitaji maalum. Katika hafla hiyo Benki ya NMB ilikabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Tsh. milioni 58.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad