Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango
anatarajiwa kuzindua mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Sabasaba
Mkoani Njombe. tarehe 02 Aprili, 2022 Aidha wananchi wa mkoa huo na
mikoa ya jirani pamoja na watanzania wote wameombwa kushiriki kwenye
uzinduzi huo.
Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge kwa mwaka 2022 ni
“Sensa ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo: Shiriki kuhesabiwa, tuyafikie
Maendeleo ya Taifa”.
Akiongea na waandishi wa habari leo, tarehe
29 Machi, 2022, Jijini Dodoma, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri
Mkuu,(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi,
amefafanua kuwa pamoja na Kauli Mbiu hiyo, Mbio hizo zitaendelea
kuelimisha na kuihamasisha jamii ya Watanzania kuhusu umuhimu na
uzingatiaji wa Lishe bora, Mapambano dhidi ya Rushwa, Mapambano dhidi ya
VVU/UKIMWI, Mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya pamoja na
Mapambano dhidi ya Malaria.
Mhe.Katambi amefafanua kuwa, baada
ya Uzinduzi huo, Vijana sita walioandaliwa kutoka Tanzania Bara na
Tanzania Zanzibar, watakabidhiwa jukumu la kuukimbiza Mwenge wa Uhuru
katika Mikoa 31 na Halmashauri 195 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa siku 195. Ameongeza kuwa, Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea
kuhamasisha wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao katika kubuni na
kutekeleza shughuli za maendeleo.
“Mwenge ni jicho la Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan, katika maeneo ambayo kote ana vyombo, anatawala na
anamifumo ya kiserikali, hilo ni jicho la ziada, kote unakopita unakagua
shughuli za maendeleo na unamulika miradi kwa kuangalia fedha
zimetumika kama zilivyo pangwa na kama haijatekelezwa ipasavyo hatua
stahikli zinachukuliwa” Mhe. Katambi
Amefafanua kuwa, Mwenge wa
Uhuru na Mbio zake umeendelea kuwa muhimu kwa taifa kwa kujenga undugu,
umoja, mshikamano na kudumisha amani pote unapopita bila kujali itikadi
za kisiasa, dini wala makabila. Aidha, amebainisha kuwa, Falsafa ya
Mwenge wa Uhuru, ndio chimbuko la Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya
mwaka 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Mwaka 1964 na Azmio la
Arusha la mwaka 1967.
Mhe. Katambi, amesisitiza kwa upande wa
Kimataifa, Mwenge wa Uhuru umeendelea kusimamia dhana yake ya kumulika
hata nje ya mipaka yetu kwani Tanzania imeendelea kuhamasisha amani
ndani ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Jangwa la Sahara na Afrika na
Duniani kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuwa msuluhishi wa amani Afrika
na imeshiriki katika ukombozi wa Bara la Afrika.
Mwenge wa Uhuru
ambao kwa mwaka huu utaanza Mbio zake Mkoani Njombe tarehe 02 Aprili,
2022 unatarajiwa kufikia Kilele chake Mkoani Kagera tarehe 14 Oktoba,
2022. Mwenge huo uliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere mwaka 1961.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe, Patrobas Katambi, akiongea na waandishi wa habari leo, tarehe 29 Machi, 2022, Jijini Dodoma kuhusu uzinduzi wa Mbio za Mwenge Mkoani Njombe tarehe 2 Aprili, 2022.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu)
Prof. Jamal Katundu, akiongea na waandishi wa habari leo, tarehe 29
Machi, 2022, Jijini Dodoma kuhusu uzinduzi wa Mbio za Mwenge Mkoani
Njombe tarehe 2 April, 2022. Kulia kwake ni Mhe. Naibu Waziri wa Ofisi
hiyo, Patrobas Katambi na Kushoto Kwake ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya
Maendeleo ya Vijana Nd. Eliakim Mtawa.
No comments:
Post a Comment