WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema sekta ya madini imeendelea kukua kwa kasi
na kuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa ambapo hadi sasa
imechangia asilimia 7.9 ya pato la taifa.
Waziri Mkuu ameyasema
hayo leo (Jumatano, Februari 23, 2022) wakati akifunga Mkutano wa
Kimataifa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania wa mwaka 2022,
uliofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere,
jijini Dar es Salaam.
Amesema mchango huo umetokana na jitihada
zilizofanywa na Serikali ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa
madini, ushirikiano baina ya wadau pamoja na sera nzuri na mazingira
rafiki yaliyowekwa na Serikali kwa wawekezaji.
“Kuimarika kwa
utendaji pamoja na mambo mengine kumekuwa ni chachu ya mafanikio hata
sasa sote tumeshuhudia kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini katika
Pato la Taifa hadi kufikia asilimia 7.9,” alisema Majaliwa na kuongeza:
“Nitoe
wito kwa watendaji wote wa sekta ya madini kuongeza juhudi katika
utendaji wenu ili sekta hii iweze kuimarika zaidi na hatimaye iweze
kuvuka lengo la asilimia 10 ya pato la Taifa ifikapo 2025 kama
ilivyobainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Majaliwa
amesema kuwa lengo la Serikali ni kutumia rasilimali ya madini kwa
manufaa ya nchi na kuboresha uendeshaji wa shughuli za madini hapa
nchini. “Ili kufikia lengo hilo, ni dhahiri kuwa ipo haja kubwa ya
kujenga mazingira wezeshi ili sekta hii iweze kuimarika zaidi kwa
manufaa ya nchi yetu.”
Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa,
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan,
anapenda kuona sekta ya madini inakuwa nguzo muhimu ya uchumi wa nchi na
ndio maana ameendelea kuipa umuhimu wa kipekee sekta hiyo kwa kutoa
miongozo ambayo imeendelea kuiboresha sekta hiyo ya madini.
“Kipekee
nimpongeze sana Rais kwa kuendelea kuhakikisha kuwa wadau wa sekta ya
madini, wawekezaji na wachimbaji wadogo wanapata huduma kupitia
maelekezo yake. Hii ni dhamira ya dhati ya Serikali yake ya awamu ya
sita katika kukwamua na kuendeleza sekta hii.”
Waziri Mkuu
ameipongeza Wizara ya Madini, kwa kuendelea kuandaa makongamano
yanayowakutanisha wadau wa uchimbaji wa madini na Serikali, jambo ambalo
limechangia kukua kwa sekta hiyo na kutoa wito kwa Wizara kuhakikisha,
inaongeza jitihada na kupanua wigo wa ushirikiano baina ya wadau na
Serikali.
Aidha, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya madini iendelee
kuimarisha mifumo ya mawasiliano na wadau wa madini ili iweze
kushughulikia kero zinazojitokeza na kuzitatua kwa wakati.
Waziri
Mkuu amesema Serikali itaendelea kuboresha taasisi zilizo chini yake
ili ziweze kutoa huduma nzuri zaidi kwa wachimbaji ikiwa ni pamoja na
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuendelea kuongeza mitambo ya
kuchorongea miamba ambayo itatoa huduma za uchorongaji miamba kwa
wachimbaji wadogo kwa bei nafuu pamoja na kuimarisha masoko ya madini
nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Dotto Biteko
amesema Wizara hiyo itaendelea na usimamizi na uratibu wa shughuli zote
za uchimbaji wa madini pamoja na kushirikiana na wadau ili kuhakikisha
sekta hiyo inawanufaisha Watanzania.
Awali, akitoa
salamu kwa uwakilishi wa Mawaziri Waalikwa kutoka Nje ya Nchi, Waziri wa
Nishati na Madini wa Burundi Ibrahimu Uwizeye, amesema Serikali ya
Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika sekta ya madini na Tanzania
imekuwa darasa kubwa kwa nchi jirani kutokana na mafanikio makubwa
yaliyotokana na uchimbaji wa sekta ya madini.
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga Mkutano wa Nne wa
Kimataifa wa Sekta ya Madini, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
cha Julius Nyerere, jijini Dar es salaam,
Baadhi
ya washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Sekta ya Madini wakimsikiliza
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua mkutano huo kwenye Kituo
cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Thursday, February 24, 2022

SEKTA YA MADINI IMEENDELEA KUIMARIKA – MAJALIWA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment