HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 1, 2022

PROF, MAHOO AITAKA KAMPUNI YA GOPA CONTRACTORS KUREKEBISHA KASORO UJENZI WA BWAWA LA ENDAGAW.

 

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Prof, Henry Mahoo amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya GOPA CONTRACTORS kurekebisha kasoro alizobaini wakati wa zoezi la kukagua ujenzi wa tuta la Bwawa la kuhifadhi maji yanayotumika kwa shughuli za Umwagiliaji katika Skimu ya Endagaw iliyoko Wilayani Hanang Mkoani Manyara.

Akizungumza katika eneo hilo, Prof, Mahoo amemuagiza Mkandarasi GOPA CONTRACTORS kuziba maeneo yanayovujisha maji katika Bwawa hilo vinginevyo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji haitapokea mradi huo.

Aidha Prof, Mahoo ametumia muda huo kutoa elimu ya ada na tozo za Umwagiliaji kwa Viongozi wa Skimu hiyo, baada ya kujionea Mkulima mmoja wa kabichi pembezoni mwa Skimu hiyo akiondoa mazao yake shambani bila kulipia gharama za Ada na Tozo za Umwagiliaji mbele ya viongozi wa Skimu hiyo.

Kwaupande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uendelezaji Miundombinu Kimasa Ntonda, amemuagiza Mkandarasi awasilishe mpango kazi mpya wa utekelezaji mradi huo utakaoonyesha namna alivyojipanga kutekeleza mradi huo na kuukamilisha kwa wakati kwa mujibu wa Mkataba ambapo pia amemshauri kazi zote zinazoweza kutekelezwa kwa wakati mmoja zifanyike ili kufidia muda uliopotea baada ya mkandarasi huyo kuchelewa kuanza kazi ya ujenzi wa Bwawa hilo kwa miezi miwili.

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilisaini makubaliano na kampuni ya Gopa Contractors ya jijini Dar es Saalam, kujenga Mfereji mpya wenye urefu wa Mita Elfu mbili na Mianne (2,400) sanjari na kuongeza urefu mfereji wa zamani kwa kujenga Mita Miasaba na Sabini (770) pamoja na kuondoa tope ndani ya bwawa linalotumika kumwagilia Skimu ya Endagaw.

Mkataba wa ujenzi wa miundombinu hiyo baina ya Tume na Mkandarasi Gopa Contractors ni wa zaidi ya Shilingi Milioni Miatisa Themanini.( Milioni 980) na ulisainiwa tarehe 31.08. 2021

Skimu ya Endagaw ina jumla ya Heka 230 na wanufaika Zaidi ya 100 wa kilimo cha Mahindi na Mboga mboga.

Mwenyekiti wa Bodi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Prof, Henry Mahoo akikagua Tuta la Bwawa la Umwagiliaji katika Skimu ya Endagaw iliyoko Wilayani Hanang Mkoani Manyara.

 Kaimu Mkurugenzi wa Uendelezaji Miundombinu Tume ya Taifa ya Bw, Kimasa Ntonda (Kulia) akitoa elimu kwa Viongozi wa Skimu ya Endagaw namna wanavyopaswa kushiriki katika ulinzi wa Miundombinu, Malighafi na vifaa vya ujenzi katika eneo hilo.

 

Mkulima katika Skimu ya Umwagiliaji ya Endagaw akivuna Mbogamboga aina ya Kabichi kwaajili ya kupeleka Sokoni.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad