HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 8, 2022

MAJAJI MAHAKAMA KUU YA TANZANIA WATOA SOMO UTAKATISHAJI FEDHA KWA MAHAKIMU

 Na Faustine Kapama – Mahakama, Lushoto

MAUNZO ya kuwajengea uwezo na uelewa Mahakimu Wakazi 200 yanayoendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yameingia siku ya pili leo tarehe 8 Februari, 2022 ambapo Majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania wamewapitisha washiriki kwenye mada kuu mbili muhimu zinazohusu utakatishaji fedha na urejeshaji mali zinazopatikana kwa njia ya uhalifu.

Mmoja wa Majaji hao, Mhe. Awamu Mbagwa amewaeleza Mahakimu hao kwa kina hatua zinazochukuliwa na mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania kupambana na makosa ya uhalifu wa kifedha kwa kuzingatia athali ambazo hutokea kijamii, kisiasa na kiuchumi. Majaji wengine walioshirikiana naye katika kuwawezesha washiriki hao ni Mhe. Edwin Kakolaki na Mhe. Dkt. Zainab Mango.

Akizungumzia kosa la kutakatisha fedha, Mhe. Mbagwa amesema kuwa utakatishaji fedha ni namna ya kujipatia fedha haramu, fedha ambazo hutokana na uhalifu na kutafuta njia mbalimbali kuwezesha fedha hizo zionekane kuwa ni halali.

Kwa mujibu wa Jaji Mbagwa, mtu anaweza kupata fedha haramu, lakini ili kuzihalalisha anaamua kuziwekeza ama kwa kununua hisa, kujenga nyumba au kuziingiza kwenye uwekezaji wowote wa kibiashara au viwanda, lengo likiwa kuonyesha uwekezaji huo ni halali, huku akijua chanzo cha fedha hizo ni haramu.

Amesema kuwa hapo awali chimbuko la kosa hilo lilikuwa ni kujihusisha na dawa za kulevya. Hata hivyo, Jaji Mbagwa amebainisha kuwa mabadiliko kadhaa yalifanyika ili kupanua uwigo wa kupambana na athali zinazotokana na kosa hilo na kujumuisha makosa yote ya uhalifu wa kupangwa wa kimataifa, juhudi ambazo zililenga kuwashughulikia wote wanaonufaika na mazao yanayotokana na makosa tangulizi kwa vile ilikuwa vigumu kuwapata mapapa wa uhalifu wanaojihusisha na makosa hayo.

“Ili kuendana na matakwa ya sheria za kimataifa, Tanzania ilitunga sheria ya utakatishaji fedha mwaka 2006. Kwa mujibu wa sheria hii, utakatishaji fedha ni kosa linalosimama pekee yake bila mtu kushitakiwa kwanza na makosa mengine tangulizi. Kwa hiyo, siyo lazima kuthibitisha kosa tangulizi ili kumtia hatiani mtu kwenye kosa la utakatishaji fedha,” amesema.

Sheria hiyo imebainisha makosa mbalimbali ya utakatishaji wa fedha, ikiwemo mtu yeyote atakaye jihusisha, moja kwa moja au kwa njia nyingine katika muamala unaohusisha mali itokanayo na mapato ya fedha haramu akiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu mali hiyo ni mazao yatokanayo na makosa ya uhalifu ambayo ni msingi wa utakatishaji wa fedha haramu.

Kwa mujibu wa sheria hii, kosa jingine ni mtu yeyote atakaye badili, hamisha, safirisha, pitisha mali ikiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu kuwa mali hiyo ni ya mapato yatokanayo na uhalifu ambayo ni msingi wa utakatishaji wa fedha haramu, kwa malengo la kuficha, kupoteza ukweli au chanzo halisi cha mali hiyo kuwa ni haramu au kumpa msaada mtu yeyote aliye husika katika kufanya kitendo hicho kwa lengo la kukwepa madhara ya kisheria.

Kosa jingini ni pale mtu yeyote atakaye ficha, funika ukweli, zuia upatikanaji wa ukweli, chanzo,mahali,Uhamishaji wa umiliki, mzunguko, au umiliki wa au haki kuhusiana na mali hiyo, akiwa anafahamu au anapaswa kufahamu au alipaswa kufahamu kuwa mali hiyo imepatikana kwa mapato yatokanayo na fedha haramu.

Amebainisha pia kuwa ili kuweza kupambana na makosa hayo ya uhalifu wa kifedha mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Tanzania, yaliamua kuanzisha sheria ili kukamata mali zote zinazopatikana kwa njia za kihalifu, malengo yakiwa kuondoa motisha zainazotokana na uhalifu huo na pia kuzuia wahalifu kufanya uhalifu zaidi.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Edwin Kakolaki akifafanua jambo wakati wa mafunzo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Awamu Mbagwa akielezea kosa la utakatishaji fedha alipokuwa anatoa mada kwa Mahakimu Wakazi wakati wa mafunzo yaliyoendelea leo tarehe 8 Februari, 2022 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zainab Mango akielezea jambo wakati wa mafunzo hayo.
Wajumbe wa Sekretarieti wakifuatilia uwasilishaji wa mada kutoka kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo akitoa mchango wakati wa kujadili mada zilizotolewa na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo (juu na chini) wakitoa michango yao wakati wa kujadili mada zilizowasilishwa.

Washiriki wa mafunzo wakiwa wamegawanyika katika makundi mbalimbali kujadili kwa kina baadhi ya maswali yaliyotokana na uwasilishaji wa mada.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo wakichukua kumbukumbu muhimu.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo (picha mbili za juu na mbili za chini) wakifuatilia uwasilishaji wa mada kutoka kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad