PROFESA NDALICHAKO AWAONYA WAAJIRI WA SEKTA BINAFSI WASIOWASILISHA MICHANGO KWA WAKATI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 27, 2022

PROFESA NDALICHAKO AWAONYA WAAJIRI WA SEKTA BINAFSI WASIOWASILISHA MICHANGO KWA WAKATI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, amewataka waajiri wa sekta binafsi kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ilio kuwaondoshea usumbufu pale watakapoondoka kazini waweze kulipwa stahiki zao kwa wakati.

Profesa Ndalichako alisema hayo jana alipofanya ziara katika Makao Makuu ya NSSF jijini Dar es Salaam yenye lengo la kujitambulisha tokea alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.

Alisema Mfuko upo kwa mujibu wa sheria hivyo ni muhimu waajiri wa sekta binafsi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuwapelekea michango wafanyakazi kila mwezi jambo ambalo ni takwa la kisheria.

“Niwasihi waajiri wote wa sekta binafsi waajiri kuhakikisha wanawasilisha michango ya watumishi wao NSSF kwa wakati ili pale ajira za watumishi hao zitakapofikia ukomo basi waweze kulipwa stahiki zao kwa wakati,” alisema.

Aidha aliwaomba watumishi wote wa sekta binafsi na hata wa umma kujenga utamaduni wa kufuatilia michango yao kama inawasilishwa kwa wakati ambapo sasa mifuko ya hifadhi ukiwemo wa NSSF umerahisisha upatikanaji wa taarifa kwa kutumia mifumo mbalimbali ya Tehama ambapo mwanachama anaweza kuangalia taarifa zake kwa kutumia simu ya kiganjani bila ya kufika ofisi za Mfuko.

Profesa Ndalichako aliupongeza Mfuko kwa kupata mafanikio mbalimbali ambapo aliwaomba kuongeza juhudi za kufuatilia michango ya wanachama kwani kuna baadhi ya waajiri wa sekta binafsi wana changamoto ya kutowasilisha michango ya wanachama wao kwa wakati.

Waziri Ndalichako pia alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii hasa katika kuongeza idadi ya wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.

Profesa Ndalichako alikiri kuwa ndani ya mwaka mmoja malalamiko ya wanachama wa NSSF yamepungua tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma ambapo baadhi ya wanachama walikuwa wanaomba msaada ili waweze kulipwa mafao yao.

“Ukweli ni kwamba sasa malalamiko mengi yamepungua na taarifa niliyopatiwa hali inakwenda vizuri…nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayofanya ya kuwahudumia Watanzania na kuwapa elimu ya kujiwekea akiba kwa ajli ya maisha yao ya sasa na ya baadaye,” alisema.

Hata hivyo aliuomba uongozi wa NSSF kuweka mkazo katika sekta isiyo rasmi kwa sababu ni sekta ambayo inakuwa sana hivyo waendelea kutoa elimu kwa wajasiriamali mbalimbali wakiwemo mama lishe, bodoboda, wavuvi, wakulima, wachimbaji wadogo wa madini pamoja na wajasiriamali wengine wote waweze kujiunga na NSSF kwa ajili ya kujiwekea akiba ya uzee.

Profesa Ndalichako alifurahishwa namna ambavyo Mfuko umejipanga kufikisha huduma zake kwa kutumia mifumo mbalimbali ya Tehama hatua ambayo itarahisisha zaidi upatikanaji wa huduma na kuwafikia wanachama wengi.

Kuhusu uwekezaji, Profesa Ndalichakao aliupongeza Mfuko kwa kufanya uwekezaji ambao ni moja ya jukumu lao la msingi na kwamba ameona miradi mingi wanayofanya ya uwekezaji na kuwataka miradi ambayo inachangamoto waendelee kuchukua hatua ili kuikwamua.

Awali, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Mfuko huo yanatokana na kazi kubwa inayofanywa na watumishi wa NSSF hasa katika kutekeleza majukumu ya msingi.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, alimshukuru Waziri Ndalichako na kumuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Balozi Ali Iddi Siwa, alisema Mfuko uko katika mikono salama na kwamba tayari makusanyo ya michango yanaendelea kukuwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi akieleza jambo wakati wa mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alipokutana na kuzungumza Viongozi na Watumishi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF)
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (kulia) akikabidhiwa Sheria na Miongozo ya Shirika hilo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa NSSF, Balozi Ali Siwa (katikati). Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi (kulia) akikabidhiwa Sheria na Miongozo ya Shirika hilo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa NSSF, Balozi Ali Siwa (katikati). Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bw. Masha Mshomba.
Baadhi ya wafanyakazi wakifuatilia kwa makini mazungumzo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hayupo Pichani)


 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad