HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 21, 2022

LUDEWA YAANZA MACHIMBO YA MAKAA YA MAWE

Na Damian Kunambi
Kufuatia kilio cha miaka mingi cha wakazi wa wilaya ya Ludewa mkoani Njombe juu ya uanzishwaji wa miradi ya Liganga na Mchuchuma hatimaye wilaya hiyo imeanza kuingia kwenye historia ya kuanza kwa mradi wa makaa ya mawe katika maeneo ya pembezoni.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya wawekezaji wa ndani wa kampuni ya makaa ya mawe MAXCOAL kujitokeza na kuanza uwekezaji katika kata ya Ibumi kijiji cha Masimavalafu ambacho pia kinapakana na kijiji cha Liugai cha kata ya Luilo.

Mpaka sasa kampuni hiyo tayari imeshapeleka sampuli kwa makampuni mbalimbali ambapo mapokeo yake ni mazuri na wanatarajia  kuanza usambazaji hivi karibuni ambapo kwa kila mwezi wanatarajia kuuza tani zisizopungua laki moja.
Vicent Malima ni Mhandisi wa kampuni hiyo ya makaa ya mawe amesema kwa mujibu wa wataalamu wamedai kuwa makaa yanayochimbwa wilayani Ludewa ni makaa yenye ubora wa hali ya juu kuliko makaa ya maeneo yote hapa nchini hivyo wao tayari wanamiliki eneo la ekari 25 ambazo watachimba kwa miaka isiyopungua 70.

 Aidha kwa upande wa mkurugenzi wa kampuni hiyo Deogratius Charles Amesema mradi huo ni mkubwa sana hivyo wananchi wa Ludewa na maeneo mengine wanapaswa kuchangamkia fursa mbalimbali za kibiashara pamoja na shughuli ndogo ndogo za mgodini.

"Napenda niwahamasishe wakazi wa Ludewa na watanzania kwa ujumla kuja kutumia fursa zilizopo hapa, mwamko umekuwa mdogo sana kuliko matarajio yangu kwani nili
tegemea kwa muingiliano huu wa watu fursa zilizopo zitachangamkiwa vyema", amesema Charles.

Sanjari na hilo mkurugenzi huyo amewatoa hofu madereva wanaokuja mgodini  kubeba mizigo kuwa miundombinu ya barabara ni rafiki kwani mpaka sasa wamesha pakia magari zaidi ya manne ya tani 30 na yamefika salama.

Pamoja na shughuli hizo za uchimbaji makaa kampuni hiyo tayari imeisaidia jamii inayowazunguka kuboresha miundombinu ya barabara ambapo wamechonga barabara ya kupita magari na kujenga daraja katika mto Ketewaka ambalo mpaka kukamilika kwake litatumia zaidi ya milioni 300 unaotenganisha kata ya Ibumi na Luilo.

Ikumbukwe kuwa wananchi wa wilaya ya Ludewa na mkoa wa Njombe kwa ujumla wanaendelea kusubiri kwa hamu kuanza kwa miradi mikubwa zaidi ya liganga na mchuchuma ambapo hivi karibuni msemaji mkuu wa serikali Gerson Msigwa alisema miradi hiyo ipo mbioni kuanza kwani tayari wapo katika hatua ya mwisho ya mazungumzo na muwekezaji.
 




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad